Raila aapa kushtaki Facebook na Cambridge Analytica kwa 'ushetani' zilizomfanyia uchaguzini
Na WYCLIFFE MUIA
KINARA wa upinzani Raila Odinga Jumanne alisema ataushtaki mtandao wa Facebook pamoja na kampuni ya Cambridge Analytica kwa kutumia jina lake kuendesha kampeni za ‘kishetani’ dhidi yake katika Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Akiongea na kituo cha Channel 4 News, Bw Odinga alisema kanda za video zilizosambazwa na Cambridge Analytica katika mitandao ya Facebook wakati wa kampeni zilimbandika sifa za ‘shetani muovu’ na zililenga kumharibia jina.
“Nilitamaushwa sana na hatua ya Facebook kukubali mtandao wao kutumiwa kwa njia za ukora. Nilikasirika sana na tunaendelea na mipango ya kushtaki Facebook..tutatumia mawiliki wetu nchini na wale wako nje ya Kenya,”alisema Bw Odinga.
Waziri huyo Mkuu wa zamani alikuwa anazungumza kwa mara ya kwanza tangu kufichuka kwa sakata kuhusu kampuni ya Cambridge Analytica kutumia habari za kibinafasi za watumiaji wa Facebook kuvuruga uchaguzi nchini Amerika na Kenya.
Bw Odinga alisema kampuni hiyo ilitumia mwanya wa idadi kubwa ya Wakenya wanaotumia intaneti kusambaza propaganda za kisiasa.
Taswira ya mtu katili
“Kanda ya ‘The Real Raila Odinga’ ilionyesha kuwa Raila ni mtu mwovu..katili mwenyewe,”alisema Bw Odinga.
Ripoti ya kampuni ya Privacy International ilisema kanda hizo za ‘The Real Raila Odinga’ ambazo zilimuonyesha Bw Odinga kuwa mpenda vita na asiyepaswa kukubaliwa kuongoza, ziliundwa na shirika la Harris Media.
Katika mahojiano hayo, Bw Odinga alisema Harris Media na Cambridge Analytical ni kampuni sawa jinsi zinavyofanya biashara ya kuamua matokeo ya kura.
“Azma ya kazi ya Cambridge Analytica na Harris Media, ilifadhiliwa na mteja mmoja na ililenga kutoa taswira mbaya katika kampeni.
Ufichuzi wa Kituo cha Channel 4 uliotolewa wiki iliyopita ulifichua kanda ya kampuni hiyo ikijigamba jinsi ilivyounda upya chama cha Jubilee mara mbili na kukiandikia manifesto, kukifanyia utafiti wa kisiasa pamoja na kukiandikia hotuba zake.
Ujuzi wa juu 2017
“Tulitumiwa kama majaribio katika uchaguzi wa 2013 na hatukujua jinsi ya kukabiliana na hali hiyo. Walirudi tena 2016 na raundi hii walirejea na ujuzi wa juu sana wa kuvuruga kampeni za kisiasa mitandaoni,” alielezea Bw Odinga.
Baada ya kufichuka kwa sakata hiyo, kampuni ya Cambridge Analytica ilimtimua Mkurugenzi wake Mkuu Alexander Nix, kwa tuhuma za kushindwa kulinda sera za kimaadili za kampuni hiyo.
Chama cha Jubilee kilikanusha madai ya kushirikiana na kampuni hiyo lakini naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe, alikiri kuwa kampuni hiyo ililipwa na Jubilee ili kukiunda upya wakati wa kampeni za 2017.
Cambridge Analytica inahusishwa na ushindi wa urais wa DonaldTrump nchini Amerika na kura ya Brexit Uingereza.
Facebook kwa upande wake iliwaomba watumiaji wake radhi na kusema imeweka mikakati ya kuhakikisha habari za wateja wake hazidukuliwi tena.