• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
NGOMA ITAMBE: Kivumbi kampeni za UEFA zikianza

NGOMA ITAMBE: Kivumbi kampeni za UEFA zikianza

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

LIVERPOOL wanaanza leo Jumanne kampeni za kutetea ufalme wa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kuvaana na Napoli jijini Naples, Italia.

Ni mchuano unaotazamiwa kurejesha kumbukumbu za msimu jana na kufufua uhamasa baina ya vikosi hivi vilivyokutanishwa tena katika hatua ya makundi muhula uliopita.

Miamba hawa waliokamilisha kampeni za ligi zao katika nafasi za pili wanakutana chini ya kipindi cha mwaka mmoja tangu Napoli wazamishe chombo cha Liverpool kwa 1-0. Ingawa hivyo, wote wanatarajiwa kusonga mbele katika Kundi E linalowajumuisha pia Red Bull Salzburg na Genk.

Katika mchuano wao wa ufunguzi wa Serie A dhidi ya Fiorentina, Napoli walitoka nyuma na kufunga jumla ya mabao manne na hivyo kusajili ushindi wa 4-3. Mechi iliyofuata iliwashuhudia Napoli wakizamishwa 4-3 na Juventus waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu jana.

Kiungo Dries Mertens alifungia Napoli mabao mawili katika ushindi wa 2-0 waliousajili dhidi ya Sampdoria wikendi iliyopita na hivyo kuchupa hadi nafasi ya tano jedwalini kwa alama sita, tatu zaidi kuliko Inter Milan wanaoselelea kileleni.

Wakifahamu jinsi walivyoponea chupuchupu kubanduliwa kwenye hatua ya makundi msimu jana, Liverpool watalazimika kujitahidi maradufu ili kuzuia balaa ambayo nusura iwapate kutokana na utepetevu wa kupoteza mechi muhimu za ugenini.

Mbali na kupoteza mchuano dhidi ya Napoli, Liverpool pia walikomolewa 2-0 na Red Star Belgrade kisha kucharazwa na PSG uwanjani Parc des Princes jijini Paris.

Kilichowaokoa Liverpool ni ubora wa fomu yao ya nyumbani iliyowashuhudia wakiwapepeta PSG 3-2 ugani Anfield. Afueni tele zaidi kwa kocha Jurgen Klopp kadri anavyokiandaa kikosi chake kupepetana na Napoli ni kutowajibishwa na nyota wake Mohamed Salah na Sadio Mane katika mechi zilizopita za kimataifa.

Katika kampeni za UEFA msimu jana, Salah aliwafungia Liverpool mabao matano huku Mane akipachika wavuni magoli manne. Kukosekana kwa mshambuliaji Arkadiusz Milik kambini mwa Napoli kunamsaza kocha Carlo Ancelotti katika ulazima wa kutegemea huduma za Lorenzo Insigne ambaye atashirikiana vilivyo na Fernando Llorente aliyeagana na Tottenham mwishoni mwa msimu jana.

Kwa upande wao, Liverpool watakosa huduma za kiungo Naby Keita, kipa Alisson Becker, difenda Nathaniel Clyne na mvamizi Divock Origi.

Borussia Dortmund watawaalika Barcelona nchini Ujerumani nao Chelsea wapimane ubabe na Valencia uwanjani Stamford Bridge, Uingereza.

Katika mechi nyinginezo zitakazotandazwa leo Jumanne, Salzburg watachuana na Genk, Inter Milan wavaane na Slavia Praha, Olympique Lyon waialike Zenit St Petersburg, Leipzig wamenyane na Benfica huku Ajax wakionana na Lille jijini Amsterdam, Uholanzi. Kati ya mechi zinazotazamiwa kuwa za kusisimua zaidi hapo Jumatano; ni pambano kati ya PSG na Real Madrid nchini Ufaransa huku Atletico wakiwaalika Juventus uwanjani Wanda Metropolitano, Uhispania.

Barcelona ndio wanaopigiwa upatu wa kutia kapuni ufalme wa taji la UEFA msimu huu hasa ikizingatiwa ukubwa wa uwezo wa safu yao ya uvamizi inayowajumuisha Lionel Messi, Luis Suarez na Antoine Griezmann. Ingawa hivyo, uwepo wa Sergio Aguero, Gabriel Jesus na Raheem Sterling katika safu ya mbele ya Man-.

Japo Neymar, Edinson Cavani na Kylian Mbappe wanapigiwa upatu wa kunogesha zaidi kampeni za PSG, uhusiano mbaya kati ya masogora hao huenda ukazamisha tena matumaini ya miamba hao wa Ufaransa.

Liverpool watashuka dimbani wakijivunia uongozi wa kilele cha jedwali la EPL kwa alama 15, tano zaidi kuliko wapinzani wao wakuu, Man-City.

Uwapo wa Mane, Salah, Firmino na mwanasoka bora barani Ulaya Virgil van Dijk unatazamiwa kuwatambisha Liverpool katika kundi hili na kufuzu kwa hatua ya 16-bora kwa pamoja na Napoli.

Mabingwa watetezi

Chelsea ya kocha Frank Lampard watatoa jasho na miamba wa Uholanzi Ajax, Valencia (Uhispania) na Lille (Ufaransa) katika Kundi H.

Chelsea ndio mabingwa watetezi wa Europa League.

Ajax walitinga hatua ya nusu-fainali msimu jana baada ya kuwabandua Real Madrid na wapambe wa soka ya Italia, Juventus. Ingawa hivyo, watakuwa na mtihani mkubwa zaidi msimu huu hasa baada ya kuagana rasmi na nyota tegemeo waliowatambisha muhula uliopita wakiwemo Matthijs de Ligt na Frenkie de Jong walioyoyomea Juventus na Barcelona mtawalia.

Man-City walitiwa katika Kundi C pamoja na Shakhtar Donetsk (Ukraine), Atalanta (Italia) na Dinamo Zagreb (Croatia). Vijana wa Guardiola wanapigiwa upatu wa kutawala kundi hili.

Tottenham waliokuwa wanafainali wa msimu jana wamo katika zizi gumu zaidi baada ya kupangwa pamoja na wafalme wa Ujerumani Bayern Munich, Olympiakos (Ugiriki) na Red Star Belgrade (Serbia) katika Kundi B.

Tottenham wanatarajiwa kuongozwa na wavamizi Harry Kane na Son Heung-min kumaliza kampeni za kundi hili katika nafasi ya pili nyuma ya Bayern.

You can share this post!

Mjane wa Simon Mukuha afariki wiki tatu baada ya mumewe...

Wasanii Wakristo waliokataa kutengeneza kadi za mialiko ya...

adminleo