Michezo

MAUANO: Patashika nguo kuchanika PSG na Real Madrid zikipapurana

September 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

MECHI iliyosubiriwa kwa hamu kubwa kati ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa na Real Madrid ya Uhispania itachezwa leo Jumatano, misimu miwili baada ya miamba hawa wa soka ya bara Ulaya kutiana kucha kwenye pambano la raundi ya 16-bora ya kivumbi hicho cha UEFA.

Pambano hili kubwa lina umuhimu kwa pande zote ambazo zinafahamika kwa wepesi wao wa kutumia pesa nyingi kusajili wachezaji wa haiba kubwa zaidi duniani.

Matokeo ya 2-0 msimu uliopita katika mkondo wa kwanza ugani Santiago Bernabeu yaliwapa Real matumaini makubwa ya kusonga mbele katika gozi la UEFA, lakini kichapo cha 3-1 katika mechi ya marudiano ugani Parc des Princes kiliwabandua nje mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Hiyo ilikuwa mara ya tatu mfululizo kwa PSG kuondolewa katika hatua ya 16 -bora ya UEFA licha ya kupigiwa upatu wa kuwa wagombezi halisi wa ufalme wa UEFA.

Kabla ya msimu uliopita kuanza, klabu hiyo tajiri ilikuwa imewavutia mastaa kadhaa wakiwemo Neymar Jr na Kylian Mbappe ambao walitua ugani Parc des Princes baada ya PSG kuweka mezani kima cha 47 bilioni ili kujinasia huduma zao. Tayari msimu huu, wameonja kichapo cha mapema cha 2-1 kutoka kwa Rennes, japo wanaendelea kuongoza msimamo wa Ligue 1 baada ya kushinda mechi nne kati ya tano zilizopita.

 

Beki Marcelo (kushoto) wa Real Madrid, awania mpira kutoka kwa fowadi Kylian Mbappe wakati wa mchuano wa awali wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uliowakutanisha ugani Santiago Bernabeu, Uhispania. Picha/ AFP

Kwingineko, vigogo wa soka ya Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich watakuwa nyumbani kuikaribisha Crvena Zvezda ya Serbia katika pambano la Kundi B.

Ingawa wengi wanatarajia wenyeji kuwa na kazi rahisi katika mechi hiyo itakayochezewa uwanjani Allianz Arena, Zvezda inakumbukwa kwa jinsi ilivyofaulu kuvuruga timu kubwa hapo awali, kitu ambacho wanaweza kukifanya katika kundi hili ambalo pia linawajumuisha Tottenham Hotspur na Olympiacos za Uingereza na Ugiriki mtawalia.

Mbali na historia yao ya awali, klabu hiyo imeandikisha ushindi katika mechi zao zote sita za Ligi Kuu nchini Serbia hadi kufikia sasa msimu huu.

Isitoshe, lazima ikumbukwe kwamba, Zvezda imefuzu kwa michuano hii baada ya kushinda timu zote kwenye mechi za mchujo.

Kwa upande mwingine, Bayern imejikusanyia jumla ya pointi nane katika mechi zao nne za Ligi Kuu ya Bundesliga za kwanza msimu huu, lakini wamejaindaa vyema huku wakitarajiwa kumtegemea mshambuliaji matata Robert Lewandowski kufunga mabao. Tayari straika huyo amemimina wavuni mabao saba tangu msimu wa Bundesliga uanze.

Mabingwa hao wanapewa matumiani makubwa ya kushinda mechi ya leo kutokana na sababu kwamba wamekuwa wakifunga angalau bao moja katika kila mechi zao za awali 28 za Klabu Bingwa wakiwa nyumbani.

Msimu uliopita, walibanduliwa nje na Liverpool ambao hatimaye walitwaa ubingwa wa michuano hiyo, Zvezda walimaliza wa mwisho kwenye kundi lao ambalo lilijumuisha wakati huo Liverpool, Napoli na PSG.

Licha ya kukosa huduma za David Alaba, Leon Goretzka na Niko Kovac wanaouguza majeraha, Bayern wangali na kikosi imara cha kuangamiza Red Star.

Sajili mpya

Huenda Lucas Hernandez aliyesajiliwa majuzi akapewa nafasi ya kucheza kama beki wa kushoto, akishirikiana na akina Jerome Boateng na Niklas Sule katika safu ya ulinzi.

Kadhalika, huenda Philippe Coutinho aliyeingizwa kutoka benchini dhidi ya RB Leipzig akaanza badala ya Thomas Muller. Kwa upande wa Zvezda, kocha Vladan Milojevic atamkosa mshambuliaji Tomane pekee.

Vikosi: Bayern Munich (4-2-3-1): Manuel Neuer; Benjamin Pavard, Niklas Sule, Jerome Boateng, Lucas Hernandez; Joshua Kimmich, Thiago Alacantra; Kingsley Coman, Philippe Coutinho, Serge Gnabry na Robert Lewandowski

Crvena Zvezda (4-2-3-1): Milan Borjan; Marko Gobeljic, Milos Degenek, Srdan Babic, Milan Rodic; Jose Canas, Dusan Jovancic; Ben Nabouhane, Marko Marin, Aleksa Vukanovic na Milan Pavkov.