KIBRA: Uhuru asema 'Mariga tosha'
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alikutana na mgombeaji wa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra McDonald Mariga katika Ikulu ya Nairobi na kumtakia ushindi.
Rais ambaye alikuwa ameandamana na Naibu wake William Ruto alimhakikisha Mariga kwamba anamuunga mkono katika kinyang’anyiro hicho cha Novemba 7.
“Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto leo katika Ikulu ya Nairobi alikutana na mwaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo ujao katika eneo bunge la Kibra McDonald Mariga. Alimhakikishia kuwa anamuunga mkono na akamtakia ushindi,” ikasema taarifa kutoka Ikulu ya Rais.
Bw Mariga alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale na kiranja wa wengi Benjamin Washiali, miongoni mwa wengine.
Katika mkutano huo Rais Kenya alimvisha Bw Mariga kofia nyekundu ya chama cha Jubilee, ishara ya kumpa baraka zake.
Hatua ya Rais Kenyatta kujitokeza wazi kumuunga mkono Bw Mariga kumeondoa dhana ambayo imekuwa ikienezwa kwamba uwaniaji wa mwanasoka huyo unaungwa mkono na Dkt Ruto na wabunge wanachama wa mrengo wa Tangatanga pekee.
Hii ni kwa sababu wabunge ambao hawaungi mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu wametangaza waziwazi kwamba wataunga mkono mgombeaji wa ODM Imran Okoth, “kwa moyo wa handisheki”.
Wao ni Maina Kamanda, Joshua Kutuny (Cherangany), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Seneta wa Murang’ a Irungu Kang’ata, kati ya wengine.