Habari MsetoSiasa

Kizaazaa bungeni Akothee kuingia amevalia sketi fupi

September 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MWANAMUZIKI mwenye utata Esther Akoth, maarufu kama Akothee Jumatano alisababisha kioja katika majengo ya bunge kwa kuingia humo akiwa amevalia sketi fupi.

Sketi hiyo, ya rangi ya kijani kibichi, ilikuwa haijafunika magoti kama inavyohitajika kulingana na kanuni kuhusu mavazi ndani ya majengo ya bunge.

Hali hiyo iliwatia kiwewe walinzi wa bunge wasijue namna ya kumdhibiti msanii huyo ikizingatiwa kuwa wenzao wanalinda lango kuu tayari walikwisha kumruhusu aingie.

Bi Akothee ambaye alikuwa amealikwa na Mbunge Maalum David Sankok, alikuwa amewasili bungeni “kuwasihi wabunge waunge mkono shughuli za wakfu wake za kuchanga fedha za kuwasaidia wahanga wa njaa katika kaunti ya Turkana.”

Wakati Bw Sankok alikuwa akimwelekeza katika eneo la chumba cha maakuli, mlango ulifungwa ghafla na walinzi wa kike.

Na ghafla bin vuu, walinzi wa kiume waliovalia mavazi ya kijani walifika hapo na kumzingira Bi Akothee.

Baada ya Bw Sankok kuwabembeleza walinzi hao kwa muda wa dakika kama 10 hivi, msani huyo aliruhusiwa kuingia katika chumba hicho cha maakuli na kuamriwa kuketi pembeni.

‘Funika mapaja dada’

Lakini aliambiwa kuwa sharti alijifunike mapaja yake kwa leso. Awali, Akothee alikataa kujifunika kwa leso hilo aliyopewa na mhudumu mmoja wa bunge.

Lakini alisalimu amri baada ya kubembelezwa na wabunge Rachael Nyamai (Kitui Kusini) na Soipan Tuya (Mbunge Mwakilishi wa Narok) waliomwelezea umuhimu wa wageni kuzingatia kanuni kuhusu mavazi bungeni.

Mwishowe alisalimu amri na kukubali kujifunga leso kufunika mapaja. Picha/ Charles Wasonga

Alifunga leso hiyo kabla ya kuruhusiwa kushiriki chakula cha mchana na mwenyeji wake, Bw Sankok.

Bw Akothee alikuwa ameandamana na wanaume wawili na wanawake wawili ambao walionekana kuwa wasaidizi au wahudumu katika wakfu wake, maarufu kama Akothee Foundation.

Binti wa Kiafrika

Alipokuwa akiondoka, Bi Akothee aliwaambia wanahabari kuwa hakuwa amevalia visivyo kwani “miguu ndio mirefu kama msichana wa Kiafrika.”

“Nimevalia sketi nzuri. Lakini kwa sababu miguu yangu ni mirefu kama mwanadada wa Kiafrika, walinzi hawa walidhani kuwa nimevalia sketi fupi. Hata hivyo, tumesuluhisha suala hilo kwa kutumia leso hii,” akasema.

Bw Sankok aliwashangaa wabunge wenzake kumtaka Akothee ajifunge leso. Picha/ Charles Wasonga

Alikariri kuwa alifika bungeni kuwashawishi wabunge kuunga mkono shughuli za wakfu za kutoa misaada kwa Wakenya wanaokabiliwa na baa la njaa katika kaunti ya Turkana.

“Uzinduzi wa wakfu wangu unafanyika Septemba 28 na nyote mnaalikwa. Nilikuwa hapa kwa mwaliko wa Mheshimiwa Sankok ili anisaidie kuwashawishi wenzake kuunga mkono mpango huu. Sherehe ya uzinduzi itafanyika katika Hoteli ya Weston,” Bw Akothee akasema.

Kuhutubia wanahabari

Na hapo alivunja sheria nyingine ambayo hairuhusu mtu yeyote ambaye sio mbunge kuwahutubia wanahabari ndani ya majengo ya bunge.

Lakini licha ya kufahamu sheria kuhusu mavazi bungeni, Bw Sankok alitetea Bi Akothee akisema kuwa vazi lake halikupasa kusababisha drama yoyote.

Hatimaye waliondoka bungeni. Picha/ Charles Wasonga

“Ni mimi nilimchukua kutoka ili apate nafasi kuwazungumzia wabunge kuhusu wakfu wake na kazi nzuri anayofanya katika jamii,” akasema.

Mnamo Machi 13, 2019, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alitoa amri kwamba wabunge, wanahabari na wageni hawataruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mijadala, sebule, chumba cha maakuli au vyumba vya kamati ikiwa hawajajivaa nadhifu.

Kulingana na Spika Muturi, wanaume wanapaswa kuvalia koti, tai, shati yenye mikono mirefu na longi huku wanawake wakihitajika kuvalia nguo iliyofunika sehemu zote nyeti kama vile mapaja na kifua.