Habari Mseto

Upungufu wa walimu wa Kiswahili wakumba shule za upili

March 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BARACK ODUOR

Shule za sekondari katika Kaunti ya Homabay zimekumbwa na ukosefu wa walimu wa Kiswahili.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa wasimamizi wa chama cha walimu cha KUPPET katika kaunti hiyo.

Walimu hao walilalamika kuwa ukosefu wa walimu wa Kiswahili katika kaunti hiyo ulikuwa umeathiri vibaya somo hilo.

Baadhi ya shule zina mwalimu mmoja tu wa Kiswahili ambaye hufunza madarasa yote, ilisema KUPPET.

Katibu Mkuu wa KUPPET Homa bay, Stephen Yogo alisema katika baadhi ya shule, imewabidi wanafunzi kujifunza somo hilo kwa kukosa walimu shuleni.

Alihoji kuwa suala hilo limepelekea matokeo ya wanafunzi katika somo hilo kudhoofika sana katika kaunti hiyo.

“Jinsi ambavyo wanafunzi wanapata alama za chini katika somo la Kiswahili katika mtihani wa kitaifa(KCSE) inahofisha. Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa wanafunzi wanafanya vibaya sana hali inayotokana na upungufu wa walimu wa Kiswahili,” alisema bw Yogo.

Alisema kuwa kutokana na upungufu wa walimu, kazi imekuwa nyingi katika baadhi ya shule kwa sababu huenda walimu wameshindwa kuhimili mzigo mkubwa.

Bw Yogo aliitaka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuajiri walimu zaidi wa Kiswahili katika kaunti hiyo ili kudhibiti upungufu.

Katibu huyo alisema upungufu huo ni mkubwa na kuitaka TSC kuwapa walimu wa Kiswahili kipaumbele itakapokuwa ikiajiri msimu ujao.