Makocha Wakenya 4 watafuta kujiongeza mafunzo Arsenal
Na GEOFFREY ANENE
MAKOCHA Wakenya Feisal Abdi Hassan, Beldine Lilian Achieng Odemba, Susan Wanjiru Njoki na Everline Achieng Onyango wamo mbioni kufuata nyayo za Hamisi Mohamed aliyeibuka nambari moja barani Afrika na kupata mafunzo kutoka kwa klabu ya Arsenal nchini Uingereza mwaka 2018.
Hassan, ambaye ni kocha kutoka jijini Nairobi, Odemba (kocha katika akademia ya Kariobangi Sharks), Njoki (kocha katika akademia ya Kahawa Sportive) na Onyango (kocha wa timu ya Mukuru Starlets) wako katika orodha ya makocha 16 kutoka Afrika waliochaguliwa kwa makala ya pili ya kuwania nafasi ya kuenda jijini London nchini Uingereza kunolewa na Arsenal kupitia kwa ushirikiano na kampuni ya kutoa huduma ya kifedha ya WorldRemit kupitia mpango wa Future Stars.
Jopo la majaji kutoka WorldRemit na klabu ya kukuza talanta ya Arsenal lilipitia maombi ya watu 20 walioingia nusu-fainali wakiwemo 16 kutoka barani Afrika.
Vigezo vilivyotumiwa ni kujitolea kwa kocha katika kuinua maisha ya jamii anakotoka, jinsi kazi yake imeweza kusaidia vijana katika jamii na uzito wa ombi la kocha katika kunufaisha jamii na mafunzo atakayokuwa amepata baada ya kurejea.
Makocha wote 20 waliofika nusu-fainali watazawadiwa jezi za Arsenal kwa wachezaji wanaonoa.
Kutoka orodha ya makocha 20, wanane (wanaume wanne na wanawake wanne) wataingia fainali. Hadithi zao zitachapishwa kwenye tovuti ya www.FutureStars.WorldRemit.com mwisho wa mwezi Oktoba kabla ya washindi wawili kuchaguliwa kupitia kura ya umma katika tovuti hii.
Mohamed aliibuka mshindi kwa wingi wa kura mwaka 2018 na kupata mafunzo kabla ya kurejea.
Orodha ya makocha 16 kutoka Afrika mbioni kwenye mpango wa Future Stars:
Nigeria
Uzoma Kingsley Akanador – Lagos
Ademilokun Oluwaseun David – Lagos
Chinasa Ukanda – Lagos
Towobola Grace Iyanuoluwa – Ibadan
Modupe Marilyn Jiwalde Pusmut – Jos
Kenya
Feisal Abdi Hassan – Nairobi
Beldine Lilian Achieng Odemba – Nairobi
Susan Wanjiru Njoki – Nairobi
Everline Achieng Onyango – Nairobi
Ghana
Samuel Taylor – Accra
Alhassan Iddi Manzah – Tamale-Dalun
Uganda
Bakit Isaac Agogo – Gulu
Andrew Amanya – Kabale
Nabisenke Joan – Kampala
Zimbabwe
Titus Tongesai Sanagurai – Harare
Winnet Muranganwa – Chitungwiza