• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Siogopi pingu, Sonko ajibu tuhuma za kujificha

Siogopi pingu, Sonko ajibu tuhuma za kujificha

Na WANDERI KAMAU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko, amesema uamuzi wake wa kwenda ‘chini ya maji’ ni kwa vile anataka kuwapa wapelelezi nafasi ya kukamilisha uchunguzi wao.

Bw Sonko hajaonekana kwa muda hadharani, kama ilivyo kawaida yake, hali iliyoibua maswali kuhusu ikiwa anakwepa kunaswa na Idara ya Uchunguzi wa Mashtaka ya Jinai (DCI) kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Lakini kwenye taarifa jana, Bw Sonko alisisitiza haogopi kukamatwa kwani amewahi kupitia hali kama ya sasa awali akichunguzwa kwa madai ya ufisadi.

“Sitaki kutoa taarifa yoyote ambayo huenda ikatia doa uchunguzi unaoendelea. Nilifanya uamuzi wangu binafsi kukaa mbali na makao makuu ya kaunti ya Nairobi, ili kutoonekana kuingilia mchakato wa uchunguzi,” akasema Bw Sonko.

Hata hivyo, gavana huyo alithibitisha anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa watu ambao hakuwataja, ambao alisema wanamtaka achague naibu gavana wanayempenda ili ashikilie nafasi yake endapo atashtakiwa.

Alikuwa amesema awali kwamba ataondoka mamlakani kwa hiari kwa muda kama atashtakiwa kwa ufisadi.

Amesisitiza hatamteua naibu gavana, hadi pale sheria kuhusu taratibu za uteuzi wake itapitishwa na Seneti na Bunge la Kitaifa na kuidhinishwa na Rais.

Kwa sasa, anataka wataalamu wa kisheria waeleze namna uongozi wa kaunti unafaa kuwa katika hali ambapo gavana na naibu wake hawapo.

Bila sheria hiyo kuwepo, alisema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida.

Nairobi haijakuwa na naibu gavana tangu Januari 2018 baada ya aliyekuwa Naibu Gavana Bw Polycarp Igathe kujiuzulu.

“Kama gavana aliyechaguliwa na wananchi, ningali nayatekeleza majukumu muhimu kuhusu usimamizi wa kaunti. Wananchi wanaweza kuthibitisha kwamba hakuna shughuli zozote ambazo zimekwama,” akasema.

EACC inamchunguza kuhusu utoaji zabuni ya Sh357 milioni ya uzoaji taka, kwa njia zinazodaiwa kukiuka sheria. Zabuni hiyo ilipewa kampuni 13.

Serikali ya Bw Sonko vile vile inachunguzwa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) kwa madai ya kutowasilisha Sh4.5 bilioni za ushuru.

You can share this post!

Wabunge ‘waingizwa box’ na Uhuru kuhusu malipo

NGILA: Dunia isipodhibiti teknolojia za #Deepfake,...

adminleo