Jeshi lafunga shirika la misaada linalotuhumiwa kuwasiliana na magaidi
Na AFP
JESHI la Nigeria, limefunga ofisi za shirika la kutoa msaada la Action Against Hunger (ACF), eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Inadaiwa shirika hilo liliwasiliana na magaidi.
Shirika hilo lilisema kwamba hatua hiyo itahatarisha maisha ya maelfu ya watu waliokuwa wakilitegemea kwa misaada ya kibinadamu.
Kwenye taarifa Alhamisi jioni, wakuu wa jeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria walilaumu ACF, wakidai shirika hilo kutoka Ufaransa lilipatia magaidi wa Boko Haram dawa na chakula.
“Vitendo vya usaliti vya shirika lisilo la kiserikali la Action Against Hunger viliendelea licha ya kuonywa likome kusaidia magaidi na vitendo vyao,” ilisema taarifa kutoka kwa operesheni ya jeshi dhidi ya ugaidi, Lafiya Dole.
Mnamo Alhamisi jioni, kabla ya taarifa ya jeshi, ACF ilikuwa imelalamikia kufungwa kwa ofisi zao Maiduguri na Damaturu.
“Uamuzi huo bila ilani na maelezo unahatarisha usaidizi ambao ACF inatoa katika jimbo la Borno na inakatiza misaada kwa mamilioni ya watu,” shirika hilo lilisema.
Mnamo Jumatano jioni, malori mawili ya jeshi yalivamia ofisi za ACF jijini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno na kitovu cha vita vya Boko Haram ambalo limeua watu zaidi ya 27,000.
“Walikuja na kuagiza kila mtu kuondoka. Walisema lilikuwa agizo kutoka juu,” alisema mfanyakazi mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake.
Alisema wanajeshi waliokuwa na magari ya kivita pia walifunga ofisi za shirika hilo katika jiji la Damaturu katika jimbo jirani la Yobe.
“Wanajeshi hao hawakueleza sababu ya kufunga ofisi hizo. Walituagiza tuondoke na hatukuchukua chochote,” mfanyakazi mwingine alisema na kuongeza: “Hatujui kinachoendelea.”
Mateka
Julai 2019 wafanyakazi sita wa ACF walitekwa na magaidi wa kundi la Islamic State West Africa Province (ISWAP); mrengo mmoja wa Boko Haram unaoshirikiana na kundi la Islamic State.
Wafanyakazi hao walikuwa wakirejea Damaturu na wangali mateka.
Madai ya jeshi dhidi ya ACF ndio ya ya punde kuhusu uhusiano wake na mashirika ya kutoa misaada. Mara kwa mara, jeshi limekuwa likilaumu mashirika hayo kwa kusaidia magaidi
Mnamo Desemba mwaka jana, jeshi lilisimamisha shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kuhudumu kaskazini mashariki likidai lilikuwa likiwapa mafunzo majasusi waliokuwa wakiunga Boko Haram.
Marufuku hiyo iliondolewa baada ya wakuu wa jeshi kukutana na shirika hilo.
Mnamo Agosti 2017, wanajeshi walifanya msako katika kambi ya Umoja wa Mataifa jijini Maiduguri, hatua ambayo ilishutumiwa na shirika la Amnesty International.
ACF inasema watu zaidi ya 7.1 milioni wanahitaji msaada kufuatia mashambulizi ya kigaidi huku 1.8 miongoni mwao wakiwa hawana makao.