• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Mkewe Cohen ataka aachwe huru amzike mume

Mkewe Cohen ataka aachwe huru amzike mume

Na RICHARD MUNGUTI

MJANE wa mfanyabiashara tajiri kutoka Uholanzi, Tob Cohen, anayezuiliwa katika gereza la wanawake la Langata, Sarah Wairimu Kamotho, ameomba Mahakama Kuu iamuru idara ya magereza imsindikize ahudhurie mazishi ya mumewe licha ya kukataa kuhudhuria kikao cha kusomwa kwa wosia wake.

Wosia huo ulipangiwa kusomwa Ijumaa katika ofisi za wakili wa marehemu.

Wakili Cliff Ombetta anayewakilisha dada wa Tob Cohen alisema familia haina pingamizi Wairimu kuhudhuria mazishi ya mumewe yatakayofanyika katika makaburi ya Mayahudi yaliyoko barabara ya Wangari Mathai, Nairobi.

Na wakati huo huo, ombi hilo la Wairimu liliorodheshwa kuwa la dharura.

Naibu wa msajili wa kitengo cha kesi za uhalifu, Bi Jane Kamau, aliamuru ombi hilo lisikizwe na Jaji Jessie Lesiit hapo Septemba 23, 2019 ili atoe maagizo kuhusu ombi hilo.

Katika ombi hilo, wakili Philip Murgor na George Ouma wanaomba mahakama iamuru msimamizi wa gereza la Wanawake la Langata amsindikize Wairimu kuhudhuria mazishi ya Cohen na kutoa heshima zake za mwisho.

Kuhudhuria

Wakili huyo alisema Wairimu anataka kuhudhuria mazishi ya mumewe kutoa heshima zake za mwisho.

Bi Kamau alielezwa kuwa mnamo Septemba 18, 2019, Jaji Stellah Mutuku aliamuru idara ya magereza kumpeleka Wairimu mochari ya Chiromo kuhudhuria shughuli ya upasuaji wa maiti.

Wakati wa shughuli hiyo, tofauti zilizuka kuhusu jinsi mazishi yatakavyoendeshwa, Wairimu akitaka aruhusiwe kuzika mwili wa mumewe.

Hata hivyo, baadaye pande zote ziliamua kwamba marehemu azikwe naye Wairimu aruhusiwe kuhudhuria.

Katika kesi hiyo Wairimu ameshtaki afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka ya Umma (ODPP) inayowakilishwa na viongozi watatu wa mashtaka Mabw Nicholas Mutuku, Alexander Muteti na Bi Catherine Mwaniki. Amemtaka dada yake marehemu Gabrielle Cohen kuwa mhusika.

You can share this post!

Seneta Murkomen mwingi wa bashasha baada ya kufanyiwa...

Ripoti yaanika uozo ulivyokithiri katika vyuo vikuu

adminleo