• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
Pasta Ng’ang’a ajitetea kuanika ziwa la mama kwenye runinga

Pasta Ng’ang’a ajitetea kuanika ziwa la mama kwenye runinga

Na BENSON MATHEKA

MHUBIRI mbishi James Maina Ng’ang’a wa kanisa la Neno jijini Nairobi, amejijitetea baada ya kuadhibiwa kwa kuanika ziwa la mwanamke kwenye kipindi cha mahubiri katika runinga ya kanisa lake, Sasa TV.

Pasta Ng’ang’a aliyeagizwa alipe faini ya Sh1 milioni kwa kitendo hicho, amesema hakufahamu ikiwa kuna mwanamke aliyefichua ziwa lake na hakufaa kuadhibiwa.

Akizungumzia kisa hicho, Bw Ng’ang’a alisema ni vigumu kwa watu kuelewa masuala ya kiroho kama kutimua mapepo yanayohangaisha watu.

Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CAK) ilisema kwamba, pasta huyo alikiuka kanuni za utangazaji licha ya kuonywa mara kadhaa kukoma kupeperusha kipindi chake katika muda usioruhusiwa.

Afisa wa mawasiliano wa CAK, Chimbiru Gimode, alisema Mamlaka hiyo ilitumia sheria ya mawasiliano ya Kenya kumuadhibu Pasta Ng’ang’a kwa kusababisha mwanamke kufichua sehemu za siri katika harakati za kumuombea.

Kulingana na sheria, vipindi vinavyohusisha matukio ya watu wazima vinapaswa kupeperushwa baada ya saa nne usiku watoto wakiwa wamelala.

CAK ilisema kwamba, Pasta Ng’ang’a aliendelea kuonyesha kipindi hicho kabla ya wakati huo licha ya kuonywa mara kadhaa.

“Vipindi au sinema zinazoorodheshwa kuwa za kutazamwa na watu wazima pekee hazitaonyeshwa kabla ya saa nne usiku,” inaeleza sheria.

Hata hivyo, mhubiri huyo alisema atakata rufaa kupinga uamuzi huo aliotaja kama uliotolewa na watu wasiofahamu masuala ya kiroho.

Kulinga na Bw Ng’ang’a, hana uwezo wa kudhibiti kinachotendeka wakati wa mahubiri yake ya kutimua mapepo kutoka kwa watu.

Kupunga na kufukuza pepo

Kwenye kanda ya video, Bw Ng’ang’ a alisema hakufahamu kama kuna mwanamke aliyeweka wazi maziwa yake wakati wa kufukuza mapepo.

“Juzi nililaumiwa kwa kuonyesha ziwa la mwanamke. Lakini ninawezaje kufanya hivyo na sijui kama kuna ziwa lililoonyeshwa kwa sababu sio langu?” alihoji.

Vituko vya mhubiri huyo vimekuwa vikiongezeka kila uchao na amekuwa akishtakiwa kortini. Agosti 2019 alisamehewa na mwanahabari Linus Kaikai aliyekuwa amemshtaki kwa kutishia usalama wake.

Aidha, baadhi ya washiriki wa kanisa lake wamemlaumu kwa kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu, madai ambayo amekuwa akikanusha na kulaumu mahasimu wake kwa kumsingizia.

Miezi mitatu iliyopita, alionekana kwenye kanda iliyosambazwa mitandaoni akiwatusi maaskofu wanaohudumu chini yake kwa kuwaita wajinga na takataka.

You can share this post!

Jubilee yaelezea uwezekano wa kumwadhibu Kamanda

Viongozi wamlaumu Ruto kuingilia siasa mashinani

adminleo