Viongozi wamlaumu Ruto kuingilia siasa mashinani

Na BARNABAS BII na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto, anakabiliwa na uasi baridi kutoka kwa viongozi wa mashinani katika ngome yake ya Rift Valley wanaomlaumu kwa kuingilia masuala ya kisiasa ya kaunti za eneo hilo.

Baadhi ya Wabunge wa Jubilee na madiwani wanadai kwamba Dkt Ruto amewatenga na kushirikiana na wenzao wanaotaka kuonyesha ubabe wao wa kisiasa.

“Tunataka Naibu Rais azingatie siasa za kitaifa na kutuacha tupambane na siasa za mashinani kwa sababu anakanganya wapigakura kwa kuunga baadhi ya viongozi,” alisema mbunge wa Jubilee aliyeomba tusitaje jina lake akihofia kuhangaishwa.

Alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo Agosti 2019 katika Kaunti ya Nandi, Dkt Ruto aliwataka wapigakura kuwakataa viongozi wanaoendeleza siasa za migawanyiko akisema wanalemaza maendeleo eneo hilo.

“Nimekuwa nikiwahimiza viongozi wazike tofauti zao na kushirikiana kwa sababu wako katika serikali ya Jubilee lakini wameshindwa kunisikiliza na wakati umefika wakataliwe kwenye debe wakati ukifika,” Dkt Ruto alisema alipofungua ofisi za CDF zilizoko Chesumei.

Alisema migogoro ya kisiasa baina ya wanasiasa imekuwa ikihujumu maendeleo eneo hilo licha ya serikali kuwa na sera mufti.

“Ni jukumu langu kumuunga Rais aafikie sera za Jubilee lakini inasikitisha baadhi ya viongozi wanatumia wakati wao kupigana badala ya kuhudumia umma,” alisema Dkt Ruto.

Wadadisi wa siasa eneo hilo wanasema Dkt Ruto anakosea kuingilia siasa za mashinanu wakisema zinaweza kuathiri umaarufu wake na kutatiza azima yake ya kugombea urais.

“Naibu Rais anafaa kuzingatia kujenga umaarufu wake kote nchini badala yua kushughulika na masuala ya kisiasa ya hapa mashinani,” alisema Bw Philip Chebunet, mdadisi wa siasa mjini Eldoret.

Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny amekuwa akimlaumu Dkt Ruto kwa kujaribu kutawala siasa za jamii ya Wakalenjin akidai amewapuuza.

“Kinachojitokeza kinadhihirisha kwamba Naibu Rais amewapuuza Wakalenjin na anachotaka ni kuwa Rais pekee,” alisema.

Umaarufu wa Raila

Wadadisi wanasema umaarufu wa Dkt Ruto na chama cha Jubilee eneo hilo umepungua huku wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga ukiongezeka.

Wanasema baadhi ya magavana wametangaza kuunga muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ambao Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakipuuza.

Dkt Ruto alikuwa amewavuta upande wake magavana Josphat Nanok (Turkana, ODM), Profesa John Lonyangapuo (Pokot Magharibi, chama cha Kanu) na Patrick Khaemba (Trans-Nzoia, chama cha Ford-K), lakini wamemhepa kwa sababu ‘haungi’ handisheki.

Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos ametangaza kuwa anaunga muafaka.

Vyama vya upinzani vimeanza kusajili wapigakura eneo la Rift Valley na kufungua ofisi.

Habari zinazohusiana na hii

Siasa zateka misaada

Duale ameruka Ruto?