Makala

SHANNICE WANGUI: Raha yangu ni kufikia upeo wa Shonda Rhimes

September 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

SURA na jina lake siyo geni kwa wapenzi wa tasnia ya filamu hapa nchini. Ndani ya miaka mitatu iliyopita alikuwa miongoni mwa waigizaji wa kike waliojivunia kuchota wafuasi wengi waliokuwa wakimfuatilia katika kipindi cha ‘Tahidi High’ akifahamika kama ‘Chepchumba’ ambacho hupeperushwa na Citizen TV.

Ingawa hajasomea masuala ya filamu, Shannice Wangui Gichia amejifunza jinsi ya kutumia kamera za kunasa video kwenye juhudi za kuzalisha filamu.

Tangu akiwa mdogo alidhamiria kuhitimu kuwa mwana habari ama mwanasheria bila kuweka katika kaburi la sahau mwigizaji.

”Sijapata umaarufu katika uigizaji lakini mwaka 2016 uliniwezesha kupata nafasi kuzuru nchini Italia kutegeneza filamu chini ya ushirikiano wa kundi la Great Potential African Youth na kampuni ya Cinemadamare Film Festival ya nchini humo” anasema na kuongeza kuwa baada ya kukamilisha shughuli hizo pia alipata fursa kuhudhuria hafla ya Venice Film Festival ambayo huandaliwa kila mwaka nchini humo.

Katika shughuli kutwa binti huyu ni mshirika wa kundi la Great Potential African Youth ambalo hupatikana mtaani Dandora, Nairobi.

Anasema anajivunia filamu iitwayo ”Born this Way’ aliyokuwa naibu director pia mnasa sauti walioitegeneza kipindi hicho maana ilibahatika kutwaa tuzo ya ‘Diaspora Best Film’ kwenye hafla ya Kalasha Awards jijini Nairobi.

”Kwa mara ya kwanza Great Potential African Youth ikishirikiana na Cinemadamare Film Festival tunatarajia kushiriki zoezi la kutegeneza filamu hapa nchini kuanzia mapema mwezi Novemba hadi Desemba mwaka huu,” alisema. Anadokeza kuwa kando na washirika wa makundi hayo pia wamealika waigizaji mbali mbali wa humu nchini kushiriki shughuli nzima.

Anasema wamepania kutegeneza filamu kadhaa katika Kaunti tano tofauti ikiwamo Nairobi, Nakuru, Kilifi, Kisumu na Kirinyaga.

Katika mpango mzima demu huyu analenga kushiriki filamu akipania kutinga levo ya waigizaji wa kimataifa. Kwa filamu za Hollywood analenga kufikia hadhi ya Lupita Nyong’o pia Shonda Rhimes mzawa wa Marekani.

Mwigizaji chipukizi, Shannice Wangui Gichia anayelenga kufikia hadhi ya Shonda Rhimes mzawa wa Marekani. Picha/ John Kimwere

Kwa kazi zake Shonda anasema hupenda kutazama ‘Greys Anatomy,’ na ‘Scandal’ zote TV Series na filamu iitwayo ‘The Princess Diaries Two.’ Kwa wanamaigizo wa Kinigeria (Nollywood) anadhamiria kutinga kiwango chake Genevieve Nnaji ambapo huvutiwa na filamu ya kwake iitwayo ‘Dangerous Sisters.’

Anatamani sana kushinda tuzo mbali mbali katika maigizo hasa baada ya filamu mbili alizoshiriki kuteuliwa kwenye hafla tofauti tangu aanze uigizaji. Mwaka 2017 filamu ya ‘Adhabu’ iliteuliwa kuwania tuzo kwenye hafla ya Macha Wood Festival ambayo huandaliwa katika Kaunti ya Machakos.

Msanii huyu analia na malipo duni akisema yanaponda wasanii chipukizi hali ambayo hufanya baadhi yao kusepa.

Pia anasema suala la ubaguzi miongoni mwao huchangia baadhi yao kunyimwa ajira. Kadhalika anadai gharama ya kuzalisha filamu imeibuka donda sugu kwa brandi zinazokuja.

Demu huyo siyo mchoyo wa mawaidha anahimiza wenzie watie bidii kukuza talanta zao katika uigizaji wala wasikubali ndoto zao ziangushwe na wasiowatakia mema.

Hata hivyo anatoa mwito kwa serikali ianzishe mikakati mwafaka itakayosaidia kupelekea sekta ya maigizo hapa nchini katika kiwango cha juu hapa nchini.