Watalii wafurika Kenya kuona pundamilia wa kipekee
Na GEORGE SAYAGIE
PUNDAMILIA mwenye madoadoa ya kipekee aliyenaswa na kamera siku sita zilizopita katika mbunga ya wanyamapori ya Maasai Mara sasa amekuwa kivutio kikubwa cha watalii katika mbuga hiyo.
Watalii wamefurika furifuri kumtazama mnyama huyo ambaye si wa kawaida, mwenye rangi nyeusi na nyeupe iliyochanganyika na madoadoa.
Inasemekana huenda akawa na chembechembe maalum mwilini zinazofahamika kama melanocytes ambazo huwezesha myama kupata rangi ya ngozi na nywele kama vile nyekundu, manjano, kahawia na nyeusi.
Siku ya Jumamosi, mnyama huyo alionekana akila nyasi na mamaye. Kwa mtazamo, alionekana kukerwa na migurumo ya magari na picha alizokuwa akipigwa.
Bw Antony Tira, mwanamume aliyemtambua punda huyo na kisha kumpinga picha iliyosambaa katika mitandao ya kijamii amempa jina lake ‘Tira’
Kulingana na Mwanaekolojia, Bw Par Lemein, punda aina hiyo hutambuliwa kila baada ya miaka kadhaa ila huwa nadra sana kupatika akiwa mkubwa.
“Tira ni pundamilia mwenye seli za melanini na mistari yake haikujiunda vyema kutokana na jeni zisizo za kawaida,” akasema Bw Lemein.