Habari Mseto

Kioja mzee kupashwa tohara kabla ya kuzikwa

September 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa kijiji kimoja katika Kaunti ya Murang’a waliachwa vinywa wazi baada ya mzee aliyekumbana na mauti akiwa na umri wa miaka 90 kupashwa tohara Jumatano, hii ikiwa ni baada ya ukoo wake kukataa kumzika kwa ‘kuruka’ hatua muhimu ya utamaduni wao.

Mzee Erastus Githinji aliaga dunia Septemba 23, 2019, nyumbani kwake katika kijiji cha Kiriko na mwili wake ukahifadhiwa katika mochari ya hospitali kuu ya Maragua.

Alikuwa amepangiwa kuzikwa Jumanne iliyopita, lakini jamaa na marafiki walipofika na jeneza la kumsafirishia akazikwe, kulizuka balaa wakati waliochaguliwa kumvalisha nguo kubainisha hakuwa amepashwa tohara.

Kikao cha dharura kiliandaliwa nje ya mochari hiyo kikihusisha ukoo wa Anjiru, mbari ya Kiragu ambao marehemu alikuwa mzawa, na ikaamuliwa mazishi hayo yaahirishwe hadi tambiko kadhaa za utakaso ziandaliwe kisha azikwe Jumamosi ijayo.

Msemaji wa familia hiyo Mzee Njogu Kiraita alisema, “ni laana kumzika mzee ambaye ameacha nyuma mke wa miaka 72 na watoto sita, watatu wakiwa wa kiume wa kati ya miaka 43 na 54 na ambao wamepashwa tohara kwa mujibu wa tamaduni za jamii hii.”

Alisema kwamba hatari kubwa ni kuwa, mwendazake ameacha wajukuu 12 na ambao kuna vijana sita ambao walipewa jina lake na ambao tayari wamepashwa tohara.

Faini

Alisema mke wa marehemu aliyefahamika kama Feliciana Njeri atatozwa faini ya mbuzi watatu na pombe ya kitamaduni kwa wazee wa kijamii walio karibu na familia hiyo kwa kuficha siri hiyo ya mumewe miaka hiyo yote 56 waliyoishi pamoja.

Bi Njeri aliyekuwa katika msafara wa waombolezaji alijitetea kuwa ni jukumu la mke kumheshimu mumewe na “kumwepushia aibu.”

Alisema wa kulaumiwa walikuwa ni ndugu zake, waume wa rika lake, na marafiki wa karibu.