• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:24 AM
HARAKATI ZA KUJIKIMU: Jamii ya ufugaji iliyobadili sura ya Samburu kwa kukuza mimea

HARAKATI ZA KUJIKIMU: Jamii ya ufugaji iliyobadili sura ya Samburu kwa kukuza mimea

Na SAMUEL BAYA

KAUNTI ya Samburu inajulikana sana kwa sababu ya shughuli za ufugaji na zaidi biashara ya mifugo.

Hii ni kwa sababu ya wakazi hao kujulikana kama wafugaji wa kuhamahama.

Hata hivyo, kuna taswira mpya kwa sababu jamii za sehemu hiyo zimeamua kuingilia ukulima wa mahindi na maharagwe, kilimo kinachofanya vyema kwa sasa.

Ziara ya Akilimali katika eneo la Maralal, katika kaunti hiyo iligundua kwamba wakazi wengi pole pole wameanza kuingilia ukulima, huku wakianza kuacha kutegemea mifugo katika maisha yao.

Baadhi ya mashamba tuliyotembelea yalikuwa yamejaa mahindi.

Kando kando mwa barabara inayotoka mjini Maralal kuelekea hifadhi ya Malasso, tuliona mashamba yaliyonawiri, hali iliyotulazimu kusimama na kuanza kuuliza kiini cha wenyeji hawa ambao zamani walikuwa wafugaji kuingilia kilimo.

Ziara yetu ya kwanza ilitufikisha katika kijiji cha Lepartuk Lgoos, kilomita 20 kutoka mjini Maralal. Katika kijiji hiki, tulikutana na Shekuti Lekidil mwenye umri wa miaka 30 pamoja na mkewe Lekidil Naseku mwenye umri wa miaka 29.

Wakazi hawa wako na watoto watano na ndani ya miaka mitano, wamekuwa wakilima mahindi na maharagwe na wamekuwa wakipata chakula cha kutosha.

“Katika shamba hili, sisi tunakuza mahindi na maharagwe. Mifugo wetu walikuwa wakiangamia wote kunapokuwa na kiangazi,” akasema Lekidil.

Alisema vifo vya mifugo wao vilikuwa vikiwatatiza sana hadi pale walipoamua kuwa sasa ni lazima wafanye ukulima kama njia mbadala.

Familia hiyo inamiliki shamba la ekari mbili kando ya barabara na mwaka jana pekee, walivuna magunia 50 ya mahindi na magunia 10 ya maharagwe.

“Tuligundua kwamba mara nyingine mvua inanyesha nyingi mpaka kunakuwa na mafuriko na mifugo wetu kusombwa na mafuriko.

Niliketi chini na mke wangu na kuamua kwamba mvua hiyo ni muhimu kwetu kufanya kilimo kila inaponyesha,” akasema Lekidil.

Ingawa bado huweka mifugo wachache, aliambia Akilimali kwamba lengo lao kubwa ni kuendeleza kilimo biashara kwa ajili ya kupata fedha na chakula kupitia mahindi na maharagwe.

“Mwaka jana tulipata mavuno mazuri sana ambapo tuliuza na nikaweza kununua ng’ombe watatu. Kama desturi yetu kama Wasamburu, kuwa na ng’ombe ni muhimu.

Kwa sasa ninapata maziwa lakini pia niko na chakula cha kutosha. Hivi sasa shamba langu liko na mahindi yaliyonawiri na ujio wa mvua utafanya jambo hilo kunawiri hata zaidi,” akasema.

Kilomita kadhaa tukafika katika shamba la Jonathan Lemisiro, mkulima ambaye pia ameamua kuchangamkia kilimo cha mahindi. Katika shamba lake la ekari tatu na nililojaa mahindi, alisema hakuwa na budi kugeukia kilimo cha mahindi na maharagwe.

“Kama Wasamburu, tumeamua pia kubadilika. Haiwezekani kwamba tutaendelea kutegemea mifugo ambayo wakati wa kiangazi huangamia. Kwa hivyo kile ambacho tunalenga zaidi ni kuwa mbali na ngombe, pia sasa tunafanya ukulima kujikimu na mavuno yamekuwa mazuri,” akasema.

Msimu mrefu wa mwaka katika kaunti ya Samburu huwa ni kiangazi huku kaunti hiyo ikipata mvua chache kwa mwaka.

Hatua hiyo ndiyo ambayo ilikuwa imefanya wakazi wengi kuamua kutegemea mifugo katika shughuli zao za kimaisha kila siku.

Kulingana na takwimu, idadi ya watu wa Samburu kulingana na ripoti ya mwaka wa 2009 ni 223,894.

 

Shekuti Lekidil (kulia) na mkewe Lekidil Naseku waonyesha ukubwa wa shamba lao katika kijiji cha Lepartuk Lgoos, takribani kilomita 20 kutoka mjini Maralal. Picha/ Samuel Baya

Kufikia mwaka wa 2017 idadi hiyo ya wakazi wa Samburu ilitarajiwa kupanda na kufikia watu 290,000 idadi ambayo ni kubwa kutoka ile ya watu 263,000 kufikia mwaka wa 2014

Kwa sababu ya umuhimu wa kilimo katika kaunti ya Samburu na jinsi ambavyo wananchi wameamua kushughulikia jambo hilo, serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kilimo kinaimarika katika eneo hilo.

Katika ripoti yake ya kutathmini maendeleo ya 2018-2022 (CIDP) kaunti ya Samburu imelenga kuimarisha miradi mbalimbali ya kilimo kwa manufaa ya wanannchi.

Ripoti hiyo inataja mpango wa serikali kujenga maeneo ya kunyunyuzia mashamba maji katika maeneo ya Kurungu, South Horr, Arsim, Tuum, Anderi, Waso Rongai, Lulu katika eneo bunge la Samburu Kaskazini.

Maeneo mengine ni kama vile Amaya na Seiya katika Samburu ya kati pamoja na Kibartare, Ngilai, Lkerei, Westgate, Gogoltim, Loijuk, Nkutuk e Ngiron and Sasaab katika eneo bunge la Samburu Mashariki.

Katika matumizi ya fedha ya mwaka wa 2019/2020, idara ya kilimo imetenga jumla ya Sh799 milioni huku idara ya kusimamia ustawi wa mimea ikipata kiasi cha Sh123 milioni.

You can share this post!

AKILIMALI: Somo la ujenzi lilivyowapa chipukizi ujuzi wa...

TAHARIRI: Wakulima wa majanichai wasipuuzwe

adminleo