HabariSiasa

Miguna apokea matibabu jijini Dubai baada ya maumivu kumzidi

March 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

WYCLIFFE MUIA na HARRY MISIKO

WAKILI mbishi Dkt Miguna Miguna Alhamisi amelazwa hosiptalini katika uwanja wa ndege wa Dubai, nchini Milki za Uarabuni, baada ya kulalamika kuwa alihisi uchungu mwingi mwilini.

Kwa sasa anapokea matibabu katika Hospitali ya Sheikh Rashid, ambapo alipelekwa na maafisa wa Canada katika jiji hilo.

Dkt Miguna alisema mwili wake, hasa mbavu, ulikuwa na uchungu wa ajabu baada ya kupuliziwa dawa za kumptezea fahamu, kupigwa, kuvutwa na kulazimishwa kuingia ndege iliyokuwa ikielekea jijini Dubai.

Picha mtandaoni zimeonyesha wakili huyo akiwa katika kitanda cha hospitali iliyo katika uwanja wa kimataifa wa Dubai.

Kwenye taarifa, Dkt Miguna alisema alikubaliwa kupewa matibabu baada ya kukataa katakata kuabiri ndege ya kuelekea jijini London, Uingereza, akisema maumivu yalikuwa yamemzidi.

Hata hivyo, uchunguzi wa kimatibabu, alisema, ulithibitisha kuwa maafisa wa polisi nchini Kenya walimjeruhi vibaya wakati wakimlazimisha kuabiri ndege Jumatano jioni.

“Nina uchungu mwingi sana upande wa kushoto wa kifua changu, mkono wa kulia na kushoto na miguuni,” akasema Alhamisi asubuhi.

“Ninaamini kuwa vibaraka wa serikali ya Kenya walidunga sindano yenye chembechembe hatari.”

Alisema uchunguzi zaidi kuhusu afya yake unahitaji kuondoka Dubai, “lakini inawezekana tu ningekuwa na paspoti yangu ya Kenya ambayo vibaraka hao walinyakua na kuharibu na kukaidi agizo la Jaji Kimaru.”