Habari

Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano ya mbio za dunia za magari

September 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

RAIS Uhuru Kenyatta, Ijumaa ametimiza mojawapo ya ahadi zake kuu kwa Wakenya alipotangaza kuwa mashindano ya magari maarufu kama Safari Rally hatimaye yamerejeshwa katika Kalenda ya Mashindano ya Kimataifa ya Magari (International Automobile Federation World Rally Championship).

Hii ina maana kuwa mwaka 2020 Kenya itakuwa mojawapo ya mataifa yatakayoandaa mashindano hayo ambayo yatavutia madereva mahiri kutoka mataifa kadhaa ulimwenguni.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Rais amesema kuwa mchakato wa kurejesha Kenya katika mashindano hayo umekamilika sasa baada ya taifa hili kusubiri kwa miaka 18.

“Ni furaha yangu leo kuwatangazia Wakenya na Afrika kwamba mchakato huu umekamilika na mashindano ya mbio za magari ya Safari Rally yamejumuishwa katika Kalenda ya Mashindano ya Kimataifa ya 2020. Hii ina maana kuwa kuwa mashindano hayo ya kimataifa yataandaliwa Kenya na Afrika baada ya kukatizwa miaka 18 iliyopita,” akasema Rais.

Rais Kenyatta amesema serikali yake itaendelea kufanya kazi na asasi husika kuhakikisha Mashindano ya Magari ya Safari Rally ya 2020 yanaandaliwa bila hitilafu zozote kushuhudiwa.