Watahiniwa njiapanda kuhusu amri ya Magoha
Na WANDERI KAMAU
HATIMA ya maelfu ya wanafunzi wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne katika baadhi ya shule za kibinafsi nchini haijulikani, baada ya serikali kuapa kufunga shule ambazo zitapatikana kutozingatia kanuni zifaazo za ujenzi.
Wanafunzi hao wanajitayarisha kufanya mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) baadaye mwaka huu.
Kwenye agizo kwa wakuu wa elimu wa kanda na wakurugenzi wa elimu katika kaunti, Katibu wa Elimu Dkt Bellio Kipsang alisema kuwa serikali itafunga shule zote za kibinafsi ambazo hazijasajiliwa na Wizara ya Elimu.
Agizo hilo linafuatia mkasa uliotokea Jumatatu iliyopita katika Shule ya Msingi ya Precious Talent jijini Nairobi, ambapo wanafunzi wanane walifariki baada ya mojawapo ya madarasa kubomoka.
Tangu mkasa huo, wizara hiyo imeanza msako mkali, ambapo shule kadhaa zimefungwa kwa kutozingatia kanuni zifaazo za ujenzi.
Baadhi ya shule ambazo zimefungwa kufikia sasa ni Shule ya Msingi ya St Catherine Bombolulu iliyo katika mtaa wa Kibra, Pama Academy iliyo katika mtaa wa Kangemi kati ya nyingine.
“Shule zote ambazo hazijasajiliwa na Wizara ya Elimu zitafungwa na wanafunzi wake kuwekwa katika shule za umma,” akasema Katibu.
Vilevile alisema kuwa shule ambazo zitapatikana kutokuwa na miundomsingi bora zitafungwa na kunyang’aywa vyeti vyao vya usajili.
Kulingana naye, shule nyingine ambazo zitafungwa ni zile ambazo zitapatikana kuongeza idadi ya wanafunzi wake kuliko kiwango ambacho zilikubaliwa.
Kutokana na hayo, aliwaagiza wakuu hao kufanya ukaguzi wa shule hizo katika maeneo wanakosimamia na kuwasilisha ripoti kwake kabla ya Oktoba 25, ambapo shule hizo zitafungwa.
Wizara hiyo pia imetangaza hatua kali kwa shule ambazo hazijawaajiri walimu ambao wamesajiliwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC).
Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema kuwa operesheni hiyo itaendelea hadi pale watakapohakikisha kuwa kila mwanafunzi anasomea katika mazingira salama.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wa elimu wamesema kuwa ingawa hatua hiyo ni nzuri, wizara inapaswa kuwashirikisha walimu na wazazi ili kuhakikisha haiwaathiri wanafunzi katika matayarisho ya mitihani yao.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Kenya (KEPSHA), Bw Nicholas Gathemia aliunga mkono hatua hiyo, akisema kuwa maisha ya watoto yanapaswa kupewa kipaumbele.
“Mpango huu ni mzuri, kwani unalenga kuhakikisha kuwa maisha ya wanafunzi yanalindwa. Maisha yao ni muhimu kuliko mitihani ya kitaifa. Mpango huu haupaswi kuonekana kumlenga yeyote kwani hakuna mtoto wa kibinafsi ama wa umma,” akasema.
Ni hali inayoonekana kuzua mgawanyiko kwani baadhi ya wazazi katika Shule ya Msingi ya Precious Talent wameiomba wizara kubatilisha uamuzi wake wa kuifunga.
Mtihani wa KCPE utaanza hapo Oktoba 28 hadi Oktoba 31 huku ule wa KCSE ukianza Novemba 4 na kumalizika Novemba 27.