• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
Viongozi, waumini wamimina noti nzee makanisani

Viongozi, waumini wamimina noti nzee makanisani

Na TITUS OMINDE

HUKU makataa ya kurudishwa kwa noti nzee za Sh1,000 yakitimia leo, imebainika idadi kubwa ya noti hizo zilitolewa kama mchango au sadaka katika baadhi ya makanisa mjini Elodret kwa kiasi kikubwa wikendi.

Viongozi wa makanisa kadhaa walikiri kwamba waumini wengi walitoa zaka na sadaka kwa kutumia noti hizo ambazo siku ya mwisho ya matumizi yake ni leo.

Askofu Bilioni Ebole wa kanisa la Oasis International mjini Eldoret alisema kuwa hali hiyo ilionyesha namna Wakenya walivyojitolea kutimiza makataa hayo.

“Kama kiongozi wa kanisa naona agizo hilo limekuwa baraka kwa kanisa, kwani idadi ya noti hizo ambazo zilitolewa kama sadaka ni nyingi ikilinganishwa na Jumapili nyingine,” alisema askofu Ebole.

Aliwashauri wachungaji wenzake ambao walipokea noti hizo kuziwasilisha katika benki haraka iwezekanavyo kabla wapitwe na muda.

Uchunguzi ambao ulifanywa na Taifa Leo pia ulibaini kuwa baadhi ya wanasiasa pia walitumia ibada ya Jumapili kuwasilisha noti hizo kupitia kwa michango makanisani.

Uchunguzi wetu ulibaini kuwa kulikuwa na michango mingi makanisani hapo jana ambapo wanasiasa waliwasilisha mabunda ya noti za zamani.

“Hizi noti nzee mhakikishe mmeziwasilisha benki hapo kesho (leo),” alisema mwanasiasa mmoja wakati wa harambe katika kanisa moja.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Njoroge amekuwa akishiriki kampeini ya kuhamasisha Wakenya kurudisha noti hizo katika benki ili wabadilishiwe mapema.

Noti hizo mpya zilizinduliwa wakati wa sherehe ya Madaraka kwa lengo la kupunguza visa vya pesa bandia na ulanguzi wa pesa nchini.

Kufikia mwisho wa wiki iliyopita, ilibainika bado kuna mabilioni ya pesa hizo mikononi mwa raia.

You can share this post!

Kambi achunguzwe na DCI, EACC – Wabunge

Sodoma na Gomora mitaani

adminleo