Habari

Jeshi la wanamaji lilikuwa wapi?

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

BENSON MATHEKA, MOHAMED AHMED na ANTHONY KITIMO

Wakenya wa matabaka mbalimbali waliendelea kuelezea ghadhabu yao kuhusiana na mkasa wa Jumapili alasiri ambapo mama na mtoto wake walipoteza maisha baada ya gari lao kutumbukia baharini kwenye kivuko cha feri cha Likoni, Mombasa.

Wengi walishangaa ni kwa nini maafisa wa jeshi la wanamaji hawakujitokeza kwa wakati ufaao kunusuru maisha ya wawili hao. Kambi ya jeshi la wanamaji na wapiga mbizi wa Bandari ya Mombasa wamo hatua chache kutoka kivuko hicho.

Gari walimokuwa wawili hao lilipotumbukia kwenye bahari Hindi, hakuna hatua zozote zilichukuliwa licha ya kuwepo kwa kikosi cha kudumisha usalama baharini kilichozinduliwa mwaka huu na Rais Uhuru Kenyatta mita chake kutoka kivuko hicho.

Wakazi walipokuwa wakitazama gari la Miriam Kighenda likizama, wanajeshi wa majini walikuwa wakiendelea na mazoezi ya kuadhimisha Siku ya Mashujaa Dei katika bustani ya Mama Ngina, hatua chache kutoka eneo la mkasa.

Mnamo Jumatatu, familia na wakazi walipokuwa wakilalamika, ndege za kijeshi zilikuwa zikipita eneo hilo kana kwamba hakukuwa na shida yoyote.

Jana, familia ya Bi Kighenda ililazimika kutafuta wapiga mbizi wa kibinafsi kutafuta mwili wake na wa binti yake Amanda Mutheu, baada ya kuhisi kuwa serikali ilikuwa ikijivuta kuwasaidia.

Hasira za Wakenya kuhusu mkasa huo ulivyoshughulikiwa zilimfanya msemaji wa serikali Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, kutangaza kuwa juhudi zinafanywa kutafuta mili ya wawili hao.

Kanali Oguna alisema licha ya hali mbaya ya hewa, wapiga mbizi wa jeshi la majini, Kenya Ferry Services Ltd, Kenya Ports Authority, Kenya Coast Guard Service na taasisi ya utafiti wa baharini walikuwa wakitafuta miili.

Hata hivyo, Wakenya hawakuridhishwa na maelezo ya serikali wakiilaumu kwa kukosa kuwajibika na kupuuza kilio cha familia ya mwanamke huyo.

Ilichukua muda wa zaidi ya saa 20 kwa wasimamizi wa feri kukutana na familia hiyo Jumatano tangu mkasa huo ulipotokea Jumapili jioni huku serikali ikijikanganya kuhusu kilichosababisha ichelewe kutafuta mili hiyo.

Jana, zaidi ya saa 40 baada ya mkasa huo, mabaharia hawakuwa wamefaulu kupata miili hiyo na gari hilo aina ya Isis hata baada ya shughuli katika kivuko hicho kutatizwa kwa muda huduma za shirika la Huduma za Kenya Feri (KFS) zilipositisha kwa nusu saa.

Wasimamizi wa KFS walisema walichukua hatua hiyo kuruhusu wapiga mbizi kutafuta mili lakini hadi wakati wa kwenda mitamboni jana jioni, hawakuwa wamefaulu kutoa mili ya wawili hao.

Mkurugenzi mkuu wa KFS, Bakari Gowa alikiri kwamba, walihusisha wapiga mbizi wa kibinafsi kusaidia shughuli hiyo huku msemaji wa serikali Cyrus Oguna akisema hali mbaya ya hewa ilichelewesha uokoaji.

Familia pia ililazimika kutafuta wapiga mbizi kusaidia shughuli hiyo huku mabaharia na wazamiaji kutoka Bandari ya Mombasa, Jeshi la wanamaji wakisema walitambua maeneo ambapo gari hilo linaweza kuwa chini ya maji.

“Tumetambua sehemu mbili, moja ina urefu wa kina cha futi 75, huku sehemu ya pili ikiwa na urefu wa kina cha futi 173,” Bw Gowa alisema huku akiongezea kuwa waokoaji wangechukua zaidi ya saa kufikia eneo hilo.

Aidha, Bw Gowa alisema hawawezi kutambua muda hasa utakaochukuliwa na waokoaji kuvuta gari na miili hadi ufuoni.

Alisema kama shirika, ilibidi kukatiza mikakati ya kuleta waokoaji kutoka nchi ya Afrika Kusini ambao wako na kampuni jijini Mombasa akisema mikakati hiyo ingechukua muda mrefu.

“Zoezi hili limechukua muda mrefu baada ya kuzingatia usalama na shughuli za feri, tumeanzisha shughuli za uokoaji mchana kwa kuepuka nyakati ambazo kuna watu wengi wanaotumia feri,”alisema.

Aliwaomba wakazi kuwa na subra akisema zoezi hilo lilihitaji shughuli za feri kusitishwa ili kuwapa usalama wapiga mbizi hao.

Aliongezea kuwa baada ya kutambua sehemu gari hilo lilipo, shughuli ya kutoa mili itaanza akisema kuwa wataipatia miili kipaumbele kulingana na hali itakavyokuwa.

“Ikiwa wataweza kutoa mili na gari tutafanya hivyo lakini tutaipa miili kipaumbele,”alisema.

Hali duni ya feri zinazotoa huduma katika kivukio cha Likoni, Mombasa imezua maswali mengi nchini ikizingatiwa mamilioni yanayotengwa kwa kununua vipuri na kuzirekebisha hutengwa kila mwaka wa kifedha.

Gari la Bi Kigenda lilitumbukia majini baada ya kurudi nyuma likiwa ndani ya feri.

Hakuna juhudi zilizochukuliwa kuokoa mwanamke huyo na binti yake hadi wakazama huku wakazi wakirekodi mkasa hao kwa simu zao.

Ilibainika kuwa licha ya kushughulikia watu zaidi ya 300,000 na magari zaidi ya 6,000, katika kivuko cha Likoni, shirika hilo halina vifaa na wataalamu wa uokoaji.