• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Waliofurushwa Mau wapewe ardhi – Wabunge

Waliofurushwa Mau wapewe ardhi – Wabunge

NA VITALIS KIMUTAI

VIONGOZI kutoka Kaunti ya Bomet wametoa wito kwa serikali kutwaa ekari nyingi za ardhi ambazo zilitolewa kwa familia za wanasiasa mashuhuri baada ya uhuru na kuwapa watu wanaofurushwa kutoka msitu wa Mau.

Seneta wa Bomet Dkt Christopher Langat, Mbunge Mwakilishi wa Kike Joyce Korir, Mbunge wa Bomet Mashariki Beatrice Kones na mwanasiasa Richard Yegon walisema kuna ardhi kubwa inayomilikiwa na familia moja mashuhuri ambayo haitumiki katika Bonde la Ufa na inafaa kugawiwa wahanga hao wa Mau.

“Huku zaidi ya watu 60,000 katika msitu wa Maasai Mau unaopatikana Narok Kusini wakikodolewa macho na ukosefu wa makao, serikali inafaa kutwaa vipande vikubwa vya ardhi vinavyomilikiwa na familia za wanasiasa mashuhuri na kuwapa watu hao,” akasema Dkt Langat.

Seneta huyo alifunguka na kusema familia hiyo inamiliki ekari 18,000 katika Kaunti Nakuru na akapendekeza ardhi hiyo itolewe kwa wanaohamishwa kutoka Mau.

“Kwa nini familia maskini ambazo zilitoa hela zao kisha kununua mashamba Mau na hata kupokezwa hatimiliki na serikali zinafurushwa ilhali kuna wanasiasa maarufu ambao hawakununua maelfu ya ekari za ardhi wanazomiliki na hata kutozitumia kwa shughuli zozote za kilimo?” akauliza Dkt Langat.

Bi Korir naye aliitaka serikali iheshimu hatimiliki za familia zilizoagizwa kuondoka Mau ili kuepuka janga la kibinadamu itakayotokana na kufurusha kwa familia kutoka kwenye vipande vya ardhi wanavyomiliki kihalali bila mpango wa kuwapa ardhi mbadala.

“Ni vyema kwa serikali na viongozi wa kisiasa wajizuie kusababisha janga la kibinadamu kwa kisingizio kwamba wanahifadhi mazingira. Ufurushaji huu haujaidhinishwa bungeni au kwenye mkutano wa baraza la mawaziri,” akasema Bi Korir.

Bi Kones naye alisema wanaume, watoto, wanawake na wazee walioondolewa sehemu ya Mau inayopatikana Narok Kusini mwaka jana, walipitia mateso makali.

na hata baadhi yao wakaaga dunia kutokana na matatizo ya kiafya.

Aidha, Bi Kones alimlaumu Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko na Kamishina wa Bonde la Ufa George Natembeya kwa kulipiza kisasi dhidi ya jamii fulani inayoishi katika Kaunti ya Narok kwa kisingizio cha kutunza mazingira.

You can share this post!

Amerika yalalama madaktari wa Cuba wanateswa

DNA yafichua wanaopigania mtoto si wazazi halisi

adminleo