Machar kukutana na baraza la UN, AU kuhusiana na amani
Na MASHIRIKA
RIPOTI za hivi majuzi za siri zinafichua kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) na Baraza la Umoja wa Afrika (AUPSC) kuhusu Amani na Usalama liko katika hatua za mwisho za kujiandaa kukutana na kuandamana na Naibu Rais wa Kwanza Sudan Kusini, Dkt Riek Machar Teny, kuelekea jiji kuu nchini humo, Juba, kabla ya Novemba 2019.
Akihutubia chama cha SPLM/A(IO), magavana na naibu mwenyekiti, Bw Henry Odwar, Dkt Machar alithibitisha kuwa UNSC itasafiri kuelekea Addis Ababa, Ethiopia, mwishoni mwa Oktoba kuandaa mkutano na AUPSC katika Mchakato wa Amani Sudan Kusini.
“UNSC itaenda Addis Ababa katika Wiki ya Tatu, Oktoba, 2019 [tarehe zitatangazwa baadaye)” ilisema taarifa kwa vyombo vya habari.
Bw Machar alithibitisha kuwa alialikwa na mashirika makuu [UNSC na AUPSC] kuhudhuria mkutano wa Baraza la Usalama jijini Addis Ababa.
“UNSC itakuwa na mkutano wa pamoja na AU na Baraza la Usalama jijini Addis Ababa. Wameniomba kukutana nao” alithibithisha Bw Machar.
Baada ya mkutano huo Addis Ababa, mashirika hayo mawili ya usalama yatasafiri hadi Juba, Sudan Kusini, kuwasilisha ujumbe imara zaidi kuhusu utekelezaji wa R-ARCISS ambapo Machar ameagizwa kuhudhuria.
Itakuwa mara ya kwanza kwa UNSC kufanya ziara kama hiyo kukutana na AUPSC barani Afrika kuhusu utekelezaji wa Amani Sudan Kusini.
Shinikizo hilo jipya la mwisho linaongozwa na Afrika Kusini iliyorejelea urais wa UNSC mwezi uliopita, Oktoba.
Rais mpya wa Afrika Kusini wa UNSC anaahidi kuangazia utekelezaji wa R-ARCISS iliyotiwa saini zaidi ya mwaka mmoja uliopita lakini inayozidi kulegea katika sekta nyingi ambazo zingepaswa kukamilishwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita tangu ilipoanzishwa.
Mnamo 2016, UNSC, AU na TROIKA zilifanya shinikizo sawa na hili dhidi ya Dkt Machar, anayeshikilia ushawishi muhimu kwa amani Sudan Kusini. Hata hivyo mashirika hayo ya ulimwengu yalitazama kwa mshtuko wakati vita vilipozuka tena miezi michache baadaye katika jiji kuu la Juba.
Bado inasubiriwa kuonekana jinsi eneo hilo, AU, TROIKA na jamii ya kimataifa zinavyojiandaa kuhakikisha enzi za giza za 2016, zilizorejesha taifa hilo vitani, hazitarejelewa tena safari hii huku Novemba ikijongea.