Habari

'Waelezea jinsi kucheleweshwa kwa uopoaji miili kunavyoathiri biashara'

October 2nd, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

SERIKALI sasa inalaumiwa kwa jinsi inavyoshughulikia jitihada za uopoaji wa miili ya Bi Miriam Kighenda na mwanawe Diana Mutheu waliotumbukia katika kivuko cha feri cha Likoni mnamo Jumapili.

Shughuli za feri zimesitishwa kwa muda wa saa tatu leo Jumatano na Waziri wa Uchukuzi, James Macharia amemteua katibu Esther Koimett kuongoza jitihada za kuopoa miili – ya mama na mwanawe – na vilevile gari lililotumbukia majini Jumapili.

Wafanyabiashara mjini Mombasa wameikashifu hatua ya shirika la feri kukatiza usafiri kwa zaidi ya saa mbili, wakisema hatua hiyo itaathiri biashara zao pakubwa.

Wengi wao ni wauzaji katika vibanda vya mboga eneo la Likoni, na wahudumu wa usafiri wa umma, na wamesema usitishaji huo unalemaza biashara zao.

Wafanyabiashara ya matatu katika barabara ya Mombasa-Lungalunga-Kwale, wamesema wamepoteza maelfu ya pesa.

Aidha wamewashauri shirika hilo kuwaruhusu kutumia kivuko cha feri cha Mtongwe.

“Tunafahamu kuwa kukatiza shughuli za vyombo hivi ni kuwapa nafasi muafaka waokoaji,lakini hatua hii inaathiri biashara zetu,” amesema Mejumaa Mwangemi anayeuza bidhaa katika kibanda eneo la Likoni.

Wakati huo huo, wamelaumu serikali kwa kuchelewesha ujenzi wa kiegesho cha pantoni cha Mtongwe.

Kituo cha feri cha Mtongwe kilifungwa Agosti 2019 na kinatazamiwa kurudia shughuli zake Machi 2020.

Na shughuli za uchukuzi ziliporejelewa, kumekuwa na hali ya mshikemshike wengi waking’ang’ania nafasi katika feri.

Muhudumu wa matatu katika barabara kuu ya Mombasa-Lungalunga Bw John Mwangi amesema muda wa saa kadhaa kusitishwa huduma  kumewafanya kupoteza abiria wengi.

“Imebidi tupunguze tripu na kufanya hivi kumetunyima fedha za kutosha. Ikifika jioni, tunafunga kazi lakini pesa haziridhishi na tajiri pia anataka,” alisema.

Aidha wameiomba serikali kuharakisha shughuli za kuopoa miili ya Bi Miriam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu, waliyotumbukia baharini siku ya Jumapili baada ya gari lao lililokuwa ndani ya chombo cha feri kuridi nyuma.

Mwingine; Bw Fadhili Hamisi ameikashifu serikali kwa kutodadarukia shughuli ya uopoaji.

Msemaji wa serikali kanali mstaafu Cyrus Oguna akihutubia wanahabari katika kivuko cha feri cha Likoni amesema wamelazimika kusitisha shughuli za usafiri wa feri ili kuwapa usalama wanaoendeleza shughuli za uokoaji.

“Tunatambua shughuli hii itaathiri uchumi wa Mombasa pakubwa, lakini tunapaswa kuzingatia – kila mmoja wafanyabiashara wakiwemo – kwamba kuna familia ambayo imepoteza wapendwa wake,” amesema Oguna.

Hata hivyo, amehakikishia Wakenya kuwa ana imani shughuli hiyo itakamilika karibuni.