Wauguzi wakubali kurejea hospitalini
Na LUCY MKANYIKA
WAHUDUMU wa afya kaunti ya Taita Taveta hatimaye walirejea kazini Jumatano, baada ya viongozi wao kuafikiana na serikali hiyo Jumanne jioni.
Viongozi hao walifanya majadiliano ya faragha na maafisa wa serikali ya kaunti hiyo wakiongozwa na naibu gavana, Bi Majala Mlaghui.
Serikali iliahidi kulipa mishahara ya wahudumu hao kabla ya tarehe 5 ya kila mwezi.
Wahudumu hao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara yao kila mwezi.
Vilevile, walikubali kulipa marupurupu yao na fedha za NHIF na NSSF.
Kabla ya kuanza mgomo wao, wahudumu hao vwakilalamikia serikali hiyo kukosa kulipa mikopo yao ya benki kama inavyotakikana.
Hata hivyo, wiki iliyopita idara ya Fedha ililipa deni la karibu Sh26 milioni kwa mashirika na vyama vya wahudumu hao.