Mwanamume, 51, akatwa sehemu nyeti na wenzake akiwa usingizini

Na NDUNGU GACHANE

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 51, amelazwa katika hospitali ya Murang’a Level Five, baada ya kukatwa sehemu nyeti na wenzake wawili aliokuwa amelala nao katika nyumba ya mmoja wao.

Kulingana na wakazi, mwanamume huyo aliungana na marafiki wake wawili kwenye kilabu kimoja katika kituo cha kibiashara cha Kamahuha mwendo wa saa mbili usiku, ambapo walikunywa pombe hadi saa nane usiku,kabla ya kuelekea kulala kwa boma la mmoja wao.

Baada ya kulala katika nyumba ya rafiki yao, mwathiriwa aliamka na kupata sehemu zake za siri zilikuwa zimekatwa na korodani kuharibiwa vibaya.

Marafiki wake walikuwa wametoroka na akalazimika kupiga kamsa kuomba msaada kutoka kwa wakazi ambao walimuita diwani wa eneo hilo kumpeleka kituo cha polisi cha Saba Saba kabla ya kukimbizwa hospitali ya Murang’a Level Five kutibiwa.

“Alikuwa katika hali mbaya, alikuwa akivuja damu nyingi na suruali yake ilikuwa umeraruliwa kutoka nyuma. Tulimuita diwani wa eneo hili ambaye alitumia gari lake kumpeleka kituo cha polisi kabla ya kukimbizwa hospitali,” alisema mkazi, Bw Nixon Warui.

Mkuu wa polisi eneo la Murang’a South, Bi Dorothy Gaitenga, alisema mshukiwa mmoja alikamatwa kufuatia kisa hicho na anawasaidia polisi katika uchunguzi.

Habari zinazohusiana na hii