Familia yaendelea kusubiri, hali ya hewa ikilemaza uopoaji
MISHI GONGO na HAMISI NGOWA
HALI mbaya ya hewa ililemaza shughuli ya uopoaji inayoendelea katika kivuko cha Likoni mjini Mombasa Alhamisi, na kuongeza mahangaiko kwa familia ya Bi Mariam Kighenda ambaye gari lake lilizama Jumapili.
Mvua kubwa na mawingu meusi yaliyotanda angani yalifanya vifaa vya kielektroniki kukosa uwezo wa kuona chini ya bahari.
“Vifaa tunavyotumia havionyeshi chini ya bahari kufuatia giza totoro na mawimbi makubwa yaliyoko chini ya maji kufuatia mvua na matope,” alisema msemaji wa serikali Cyrus Oguna.
Wakati huo huo Bw Oguna alisema kuwa serikali haitahusisha waokoaji kutoka nchi za kigeni akihakikisha kuwa waokoaji wa jeshi la wanamaji wana ujuzi na tajriba ya kutosha kukamilisha zoezi hilo.
Bw Oguna pia alisema raia yeyote atakayetaka kusaidia katika zoezi hilo lazima afuate amri za jeshi la wanamaji ili kuwe na utaratibu katika shughuli hiyo.
Alikanusha kuwa gari la Bi Kighenda lilielea kwa muda wa dakika 20 kabla ya kuzama.
“Gari lilichukua dakika moja na sekunde 24 kabla ya kuzama baharini, hivyo madai kuwa lilichukua muda mrefu ni pang’ang’a tu zinazoendelezwa na watu ili kutoa lawama zisizostahili,” alisema.
Mwenyekiti wa Shirika la Huduma za Feri, Bw Dan Mwazo, aliomba wanaotumia kivuko hicho kufuata sheria za shirika hilo akisema ajali nyingi zinazotokea katika kituo hicho husababishwa na abiria kutozingatia sheria za usalama zilizopo.
Zoezi la uopoaji linaendelezwa na shirika la huduma za feri KFS, Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA), kikosi maalum cha ulinzi baharini, KCGS na taasisi ya utafiti wa baharini walikuwa wakitafuta miili.
Jana ikiwa ni siku ya tano tangu gari la Bi Kigenda kutumbukia majini baada ya kurudi nyuma likiwa ndani ya feri.
Mbunge wa Likoni , Bi Mishi Mboko aliiomba serikali kutengea shirika la feri pesa zaidi zitakazoliwezesha kununua vifaa muafaka vitakavyotumika kukabiliana na matukio ya ajali katika kivuko hicho mara kwa mara.
Aidha aliwataka maafisa katika jeshi la wanamaji kuhakikisha wanashughulikia ajali mara moja wanapoitwa na kuepuka kuchukua muda wakisubiri amri kutoka kwa wakuu wao.
Kwingineko, baadhi ya wazee wenyeji wa Likoni walitoa kauli yao na kusema kuna haja ya tambiko kufanywa eneo hilo.
Wazee hao kutoka sehemu tofauti za eneo hilo, walidai majanga ya watu kuzama na magari kutumbukia baharini yanayoshuhudiwa mara kwa mara kivukoni hapo yanatokana na majini na pepo wabaya.
Walisema njia pekee ya kuepusha majanga ya aina hiyo katika siku zijazo, ni kwa jamii pamoja na wahusika wa serikali na Shirika la Kenya Feri, kukubali mila na tamaduni ambazo wazee walikuwa wakizitekeleza.
Mzee Mwinyi Hamisi Mwakinyasi,76, almaarufu Mwapojjo, na mkazi wa mtaa wa Mshale, jana aliliambia Taifa Leo kuwa kupuuzwa kwa mambo ya kimila na itikadi za kale kunachangia visa vya majanga katika kivuko hicho.