• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Joho sasa akutana na Matiang’i kuzima hasira kuhusu SGR

Joho sasa akutana na Matiang’i kuzima hasira kuhusu SGR

Na CECIL ODONGO

SERIKALI jana iliwahakikishia wakazi wa Pwani kwamba agizo la usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa ya SGR kwa lazima bado limefutiliwa mbali hadi maelewano kuhusu masuala tata yaafikiwe.

Waziri wa uchukuzi James Macharia alitoa tangazo hilo baada ya kuongoza mkutano na viongozi wa Pwani, kikao ambacho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

“Kumekuwa na hofu kwamba serikali imeregesha agizo la kuwaamrisha wafanyabiashara wote kusafirisha mizigo yao kupitia SGR lililotolewa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru(KRA) na Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA).

“Hata hivyo, natangaza hapa mbele ya viongozi hawa kwamba agizo hilo halijakuwa likitekelezwa na halitatekelezwa hadi mashauriano kuhusu maswala yaliyoibuliwa yakamilike,” akasema Dkt James Macharia.

Waziri huyo pia alisema kwamba uongozi wa KPA na SGR lazima ushirikiane pamoja, akishikilia kwamba wafanyabiashara kwa sasa wanaweza kukumbatia mbinu zozote kusafirisha mizigo yao.

Kumekuwa na maandamano na malalamishi kutoka kwa wafanyabiashara na wakazi wa Pwani kwamba uchumi wa eneo hilo unaendelea kuzorota na kazi zinaendelea kuadimika kutokana na agizo hilo tata la kuwashurutisha kusafirisha mizigo kupitia SGR kutoka Mombasa hadi Kituo Kikuu cha makontena cha Embakasi.

“Lengo la serikali ni kustawisha mji wa Mombasa ili upande hadhi na kufikia kiwango cha kimataifa kutokana na umuhimu wake wa kibiashara nchini. Hakuna kilichobadilika na usafirishaji wa mizigo utaendelea kama zamani,” akaongeza baada ya mkutano jumba la Harambee.

Dkt Matiangi naye aliwashukuru Bw Joho, Seneta Mohamed Faki na wabunge kwa kukumbatia mazungumzo kuhusu suala hilo.

You can share this post!

Familia yaendelea kusubiri, hali ya hewa ikilemaza uopoaji

Waahirisha mazishi hadi shemeji alipe deni

adminleo