ODM yamrarua Mudavadi
Na MARY WANGARI
MALUMBANO ya kisiasa kati ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, na kile cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi yaliendelea kutokota Alhamisi huku ODM ikimtaka Bw Mudavadi kujiondoa rasmi katika muungano wa NASA.
Majibizano ya maafisa wakuu wa vyama hivyo yalitokea baada ya matamshi ya Bw Mudavadi nchini Amerika kwamba, handisheki ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ilichochewa na vitisho vilivyotolewa na Amerika kwa vigogo wa kisiasa wakati wa taharuki zilizotanda baada ya uchaguzi wa urais 2017.
Akihutubia wanahabari jana Nairobi, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alimshutumu vikali kiongozi huyo wa ANC akasema hawatavumilia “uongo” unaoenezwa na Bw Mudavadi.
Kulingana naye, madai yake hayakuwa na msingi kwa kuwa Bw Mudavadi amewahi kukiri kwamba hafahamu lolote kuhusu handisheki.
“Uongo unaoenezwa na Bw Mudavadi unahitaji kupingwa kwa kila njia. Tuko tayari kutangaza rasmi talaka ya kisiasa kati yetu kwa sababu Bw Mudavadi hakutusaidia hata tulipomhitaji zaidi wakati wa kumwapisha Raila Odinga kama rais wa wananchi,” akasema.
Aliongeza kwamba, imani ya ODM kwa NASA ambayo vinara wake wengine ni Kalonzo Musyoka anayeongoza Wiper, na Musalia Mudavadi wa Ford Kenya ilipotea walipokosa kuhudhuria kiapo hicho.
Bw Sifuna alikuwa ameandamana na viongozi kadha, akiwemo Wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Kingi Michael Thoya (Magarini), Wabunge Maalumu Dennitah Ghati na Godfrey Osotsi miongoni mwa wengine.
Waliungana kumkashifu Bw Mudavadi na kudai ni mwanasiasa kigeugeu tangu jadi anayejiendeleza kisiasa kwa kutegemea jasho la wengine.
“Sifa ya Mudavadi kama mwanamageuzi wa kuyumbayumba ni ya miaka mingi ikiwemo 2002 mashujaa wa demokrasia walipoungana pamoja kuing’atua KANU. Inakumbukwa alizima simu yake dakika ya mwisho…kisha akagutuka baadaye akiimba ‘Kanu yajenga nchi,” akasema Bw Sifuna.
Alizidi kusema: “Punde baada ya handisheki, alisikika akiikashifu akisema haitaifaidi Kenya kwa vyovyote. Baadaye, aligeuza wimbo na kuanza kuiunga mkono. Inashangaza hivyo basi kumsikia nchini Amerika akisema, handisheki ilitokana na shinikizo za mataifa makuu ulimwenguni.”
ANC hata hivyo ilitaja madai ya ODM kama kasheshe tupu huku ikisema ODM inamkosea heshima Bw Mudavadi.
“Tunajutia kwamba hivi ndivyo hadhi ya uongozi imeshuka nchini mwetu. Tutajiepusha kujihusisha na vita vya maneno na ODM. Tunaamini watu wanaweza kutofautiana kwa njia ya heshima,” akasema Katibu Mkuu wa ANC, Bw Barrack Muluka.
Bw Muluka alitilia shaka uaminifu wa handisheki akiuliza inakuaje mtu aliyejiapisha kuwa rais wa wananchi, kwenda kula sahani moja kisiri na hasimu wake mkuu.
“Ulimwengu unajiuliza, ni tukio gani la kumbadilisha alilokutana nalo? Ni lini aliona mwangaza katika safari yake yenye giza kuelekea Damascus?” akasema kwenye taarifa.
Bw Osotsi, ambaye alichaguliwa na ANC, alimtaka Bw Mudavadi kuitisha mkutano wa wanachama pindi atakaporejea kutoka Amerika na kutangaza rasmi kujiondoa kwake kutoka NASA akimshutumu kwa kujifanya kiongozi wa upinzani ilhali alikuwa akishirikiana na wadau wa handisheki kisiri.
“Mudavadi anajifanya kama mpenzi aliyetemwa, na jambo la busara anachofaa kufanya ni kuondoka katika ndoa hiyo,” alisema Bw Osotsi.