Waahirisha mazishi hadi shemeji alipe deni
Na JOHN NJOROGE
KISANGA kilizuka Elburgon, Kaunti ya Nakuru wakati familia ilipoahirisha mazishi ya mpendwa wao hadi shemeji yake alipe deni la marehemu la Sh80,000.
Jamaa za mwendazake walibeba jeneza lililokuwa na mwili huo na kuliweka nje ya nyumba ya shemeji yake.
Ilisemekana kabla afariki, marehemu Ruth Wamaitha Njoroge, alikuwa ameagiza ni lazima shemeji yake alipe deni hilo lililodumu kwa zaidi ya miaka 20 kabla azikwe.
Hayo yalifichuliwa na mwanawe mwendazake, Bw Simon Njoroge.
Kulingana na nakala zilizoonwa na Taifa Leo, kiasi cha hela alizodaiwa shemeji huyo na marehemu kilikuwa Sh155,000 ambapo Sh75,000 zilikuwa zimelipwa.
“Nilikuwa mwanafunzi katika Wisdom Institute, Kinangop lakini nikaacha shule kutokana na karo ya shule,” alisema Bw Njoroge.
Waombolezaji waliokuwa wamesafiri kutoka pande za mbali kuhudhuria mazishi ya jamaa na rafiki walipigwa na butwaa wakati mazishi yalipoahirishwa katika dakika ya mwisho.
Watazamaji walifurika nyumbani kwa Bw Dancan Kuria Mbugua, shemeji yake marehemu, kushuhudia jeneza lililoachwa katika boma lake eneo la Kasarani mjini Elburgon.