• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Waziri alilia viongozi wachangie kampeni ya HIV

Waziri alilia viongozi wachangie kampeni ya HIV

Na AGGREY OMBOKI

WAZIRI wa Afya Bi Sicily Kariuki amewaomba viongozi wa kisiasa wanaume kuisaidia nchi kukabiliana na virusi vya HIV kwa kuwarai wanaume zaidi kujitokeza kukaguliwa ili kubaini ikiwa wana virusi hivyo.

Akizungumza jana kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa Kujikinga Dhidi ya Ugonjwa huo, waziri alisema kuwa wanaume wengi hawajakuwa wakijitokeza kukaguliwa virusi hivyo ikilinganishwa na wanawake.

“Tumegundua kuwa wanaume wengi huwa wanafika katika vituo vya afya wakati wanaugua. Wengi hao huenda hospitalini wakati tayari wameathiriwa vibaya na ugonjwa huo. Hali ni kinyume kwa wanawake, ambao hufika katika vituo hivyo mara nyingi kukaguliwa,” akasema.

Akaongeza: “Ningetaka kuwaomba viongozi wanaume kuwahamasisha wanaume zaidi kujitokeza kukaguliwa dhidi ya virusi hivyo.”

Kwa sasa, kuna watu 1.6 milioni nchini wanaokisiwa kuishi kwa virusi hivyo. Kulingana na wataalamu, maradhi hayo yanawaathiri sana wale walio kati ya umri wa miaka 15 na 49.

Kulingana na takwimu, watu 46,000 huwa wanaambukizwa ugonjwa huo nchini kila mwaka, huku 25,000 wakifariki kutokana na matatizo yanayohusiana nao.

You can share this post!

Sarah Wairimu akanusha shtaka la kumuua mumewe

Tabichi awapa walimu Uingereza mbinu za kufundisha

adminleo