KAULI YA MATUNDURA: Mkangi aliandika Walenisi kwa mafumbo kuepuka rungu la dola?
Na BITUGNI MATUNDURA
Riwaya ya Walenisi (Katama Mkangi) ndiyo riwaya ya ‘kwanza changamano’ kuwahi kutahiniwa katika somo la fasihi ya Kiswahili katika kiwango cha shule za upili nchini.
Katika makala yangu ‘Uhusiano wa mwandishi na mazingira aliyolelewa’ (Taifa Leo, Desemba 15, 2003), nilidai kuwa aghalabu watunzi wa kazi kifasihi huakisi tajriba zao maishani katika tungo zao.
Walenisi ni mfano mzuri ambapo Mkangi anatusawiria baadhi ya tajriba na falsafa zilizoyaongoza maisha yake katika uhai wake – lakini kwa kutumia mkwepo au fumbo.
Maswali tunayofaa kujiuliza ni: Riwaya changamano/dhati ni ipi? Kwa nini mkwepo au fumbo? Riwaya changamano ina muundo mgumu na uhitaji upevu wa akili ili msomaji aielewe.
Msuko wa riwaya hii huwa tata. Mbali na Walenisi, wahakiki wanaelekea kukubaliana kuwa tungo nyingine katika kundi hili ni Nyongo Mkalia Ini (Rocha Chimera), Ziraili na Zirani (W.E. Mkufya), Babu Alipofufuka (S.A.Mohamed), Nagona na Mzingile (E.Kezilahabi) Bina-Adamu! na Musaleo za Kyalo Wamitila.
Mwanafunzi wa fasihi hana budi kuelewa aghalabu kwa kinaganaga hulka na falsafa za Katama Mkangi ili kuielewa Walenisi. Mkangi alikuwa msomi na mkereketwa wa utetezi wa ‘ukombozi wa pili nchini’.
Kwa kuamini falsafa ya ujamaa (Socialism), tunamwona Mkangi akiuliza katika riwaya yake ya Mafuta (1984), “Ni kwa nini kuna matajiri wachache na maskini wengi katika jamii?”
Akiwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Mkangi alishirikiana na kina Ngugi wa Thiong’o, Maina wa Kinyatti, Micere Githae Mugo, Alamin Mazrui, Abdilatif Abdalla miongoni mwa wengine kushutumu utawala mbaya wa serikali ya Kanu.
Mwakenya
Mnamo mwaka 1986, alitiwa kizuizini kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa kundi haramu la Mwakenya ambalo yadaiwa lilikuwa na nia ya kuipindua serikali ya wakati huo.
Hali hii inajitokeza katika Walenisi ambapo Dzombo (mhusika mkuu) anahukumiwa kifo kwa kuingizwa katika chombo cha sayari kinachotumiwa na viongozi dhalimu dhidi ya wapinzani wa utawala wao.
Kinaya ni kwamba, chombo cha kifo kinakuwa chombo kinachomwezesha Dzombo kujifahamu zaidi, kuielewa nchi yake na kuyaelewa mazingira yake kwa undani zaidi.
Walenisi ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa fumbo. Katika miaka ya 1980 na 1990, serikali za Kenya wakati huo hazikutakakukosolewa. Wakati huo, vyombo vya dola – mathalan mahakama, magereza na polisi vilitumiwa kunyanyasa raia.
Kwa hiyo, watu wengi, wakiwemo waandishi waliogopa kukwaruzana na utawala. Mkangi aliamua kutunga Walenisi kwa njia ya fumbo ili kuepuka rungu la dola. Dzombo, anahukumiwa kifo na mahakama kwa madai kuwa kavunja sheria za nchi.
Ujasiri wa Dzombo
Baada ya kuwekwa kwenye sayari ya mauti, mahakama ilifikiri Dzombo ameangamizwa na sayari hiyo ya kifo, lakini Ddombo aliimiliki kwa uhodari na ujasiri mwingi.
Chombo hicho kinampeleka katika ulimwengu mpya unaokuwa funzo kubwa kwake – funzo analoweza kulitumia kuielekeza nchi yake katika mfumo mwingine unaolinda maslahi ya waliowengi.
Wataalamu Njogu na Chimerah wanaiona Walenisi kuwa taashira ya safari ya maisha ambapo mtu anajisaka na kujiuliza: yeye ni nani? Anatoka wapi? Anaenda wapi katika mustakabali wa jamii yake? Ni safari inayoangalia muumano wa jana (historia) leo na kesho.
Mkangi anaikamilisha hadithi yake kwa kauli kwamba, Dzombo anaamua kurudi duniani – bila shaka kuwafundisha Wanawalenisi wenzake. Je, watamsikiliza au watamkana jinsi Yesu wa Uyahudi alivyokanwa na hatimaye kuangikwa msalabani?
Aidha, Chimerah na Njogu wanaifasiri, riwaya ya Walenisi kwa misingi ya msimamo wa mshairi T.S. Elliot (1963) katika shairi lake ‘East Cocker’ kuwa mwanzo wa Dzombo ndio mwisho wake na mwisho wake ndio mwanzo wake.
Je, Dzombo atafanikiwa kuleta mageuzi?
Bitugi Matundura ni msomi, mtafiti, mkereketwa wa lugha na mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka. [email protected]