Rwanda kutua nchini kwa mchuano wa Kombe la Afrika U-20
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya soka ya Rwanda ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 itawasili Kenya Ijumaa kwa mchuano wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2019.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times, kocha mkuu Vincent Mashami atataja kikosi cha wachezaji 18 Alhamisi kabla ya timu hiyo kufunga safari ya kuelekea jijini Nairobi.
Gazeti hilo limesema kwamba Junior Wasps ilicharaza klabu ya SC Kiyovu 2-1 katika mechi ya kirafiki Jumanne uwanjani Amahoro, huku “Mashami akikiri kwamba bado vijana wake wana kazi ya kufanya mazoezini kabla ya kuwa tayari.”
Timu hiyo, ambayo itakabiliana na Kenya hapo Aprili 1 mjini Machakos na kurudiana Aprili 21 jijini Kigali, ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya klabu nyingine ya Rwanda, Police FC, Machi 24.
Mshindi kati ya Kenya na Rwanda atajikatia tiketi ya kulimana na mabingwa watetezi Zambia katika raundi ya pili mwezi Mei.
Raundi ya tatu itafanyika mwezi Julai ambapo mshindi ataungana na wenyeji Niger katika Kombe la Afrika mwaka 2019. Timu zitakazofika nusu-fainali kwenye Kombe la Afrika zitafuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini Poland baadaye mwaka 2019.