SHINA LA UHAI: Afua kwa wanaougua kansa ya mapafu
Na LEONARD ONYANGO
MATUMAINI ya wagonjwa wa kansa ya mapafu kupata matibabu yameongezeka baada ya wanasayansi kuthibitisha kuwa kifaa kipya cha kutambua matibabu wanayohitaji kinatoa matokeo sahihi kwa zaidi ya asilimia 80.
Kifaa hicho kinachofahamika kama eNose, yaani ‘pua la kielektroniki’, ‘hunusa’ pumzi ya wagonjwa na kuwaeleza madaktari ikiwa mwathiriwa wa kansa ya mapafu anastahili kupewa dawa ya kupunguza makali ya saratani, maarufu immunotherapy au la.
Kulingana na matokeo ya utafiti yaliyochapishwa katika jarida la utafiti wa kansa, Annals of Oncology, kifaa hicho kinatoa matokeo sahihi zaidi ikilinganishwa na teknolojia inayotumika sasa.
Profesa Michel van den Heuvel wa Chuo Kikuu cha Radboud cha nchini Uswisi aliyeongoza utafiti huo, alisema kifaa hicho kitaboresha matibabu ya kansa ya mapafu.
“Teknolojia inayotumika sasa kubaini aina ya dawa ambayo waathiriwa wanahitaji inachukua muda mrefu na mara nyingi haitoi matokeo sahihi,” akasema.
Immunotherapy ni dawa ambayo huongeza nguvu kinga za mwili hivyo kuziwezesha kukabiliana na makali ya kansa.
“Tangu matibabu ya haya yalipoanzishwa, ukabilianaji na kansa ya mapafu umeimarika pakubwa. Lakini changamoto iliyopo ni kwamba madaktari hawana vifaa vya kupima ili kubaini wagonjwa wanaofaa kunufaika na matibabu hayo. Hii ni kwa sababu si waathiriwa wote wa kansa ya mapafu wanaonufaika na dawa hiyo,” akafafanua Prof Heuvel.
Kulingana naye, baadhi ya wagonjwa wa kansa ya mapafu hawapati nafuu hata wakipewa matibabu haya. “Kifaa cha eNose kitawezesha madaktari kutoa matibabu ya Immunotherapy kwa wagonjwa ambao watapata nafuu pekee,” akasema.
eNose ni kifaa kilichoundwa kwa teknolojia inayotambua kemikali inayojulikana kama ‘Volatile Organic Compounds’ (VOCs), ambayo hupatikana katika pumzi.
Mbali na VOCs, pumzi pia hujumuisha hewa aina ya nitrojeni, oksijeni, kabon-dayoksaidi na maji.
Kulingana na watafiti, kifaa hiki kinapima kemikali ya VOCs na kuwaeleza madaktari ikiwa mgonjwa anahitaji matibabu ya Immunotherapy au la.
“Mgonjwa anavuta hewa kwa takribani dakika 10 na kisha kupumua hewa hiyo ndani ya kifaa cha eNose. Kifaa hiki hupima hewa hiyo na kutoa majibu ikiwa mwathiriwa anahitaji matibabu ya Immunotherapy au la,” akasema.
Kimekuwa kikifanyiwa majaribio tangu 2016 ambapo wagonjwa 143 walishirikishwa katika utafiti huo.
“Majaribio yamethibitisha kuwa kifaa hiki kinatoa matokeo sahihi na kitasaidia pakubwa katika matibabu ya kansa ya mapafu,” akasema.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 80 ya kansa ya mapafu husababishwa na uvutaji wa sigara.
Ripoti ya Wizara ya Afya iliyotolewa 2016, ilionyesha waraibu huvuta sigara katika maeneo yenye msongamano wa watu hivyo kuwatia hatarini watu wengine zaidi ya milioni 10 wasiovuta sigara.
Sigara huvutwa kwa wingi usiku katika baa na maeneo ya burudani ambapo huwa na misongamano ya watu.
“Wazazi wanapovuta sigara nyumbani pia huwatia watoto katika hatari ya kupatwa na kansa ya mapafu,” ikasema ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti, zaidi ya Wakenya 2.5 milioni huvuta sigara au hutafuna tumbako hivyo wako hatarini ya kupatwa na kansa ya mapafu.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa karibu asilimia 50 ya waraibu wa sigara walianza kuvuta wakiwa na umri wa kati ya miaka 18 na 25.
Kansa ya mapafu huua watu wengi kuliko kansa ya pumbu, korodani, sehemu ya uzazi na matiti kwa pamoja.