• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Miguu huuma wakati wa baridi, kulikoni?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Miguu huuma wakati wa baridi, kulikoni?

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Mamangu ambaye yuko katika miaka ya sitini amekuwa akikumbwa na maumivu kwenye miguu yake hasa nyakati za baridi au baada ya kufanya kazi zinazohusisha matumizi ya maji baridi. Tatizo laweza kuwa nini?

Emmy, Mombasa

Mpendwa Emmy,

Mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa yakihusishwa na uchungu hasa miongoni mwa watu wanaougua ugonjwa wa baridi yabisi (arthritis), maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo, jongo (gout), maumivu ya neva na hali zingine zinazosababisha maumivu. Hakuna ushahidi wa kisayansi kuthibitisha haya, na hivyo hakuna tiba. Unaweza kudhibiti hali hii kwa kuvalia mavazi yanayozuia baridi, kudumisha uzani unaofaa, kufanya mazoezi, kutumia dawa za kukabiliana na maumivu na kujiepusha na kazi ngumu zinazofanya neva na misuli yako kukazika.

 

Mpendwa Daktari,

Pamoja na mke wangu tumejaliwa watoto watatu. Kifungua mimba wetu alizaliwa miaka saba iliyopita, huku mtoto wetu wa pili akiwa bado hajatimu miaka miwili. Mtoto wetu wa tatu alizaliwa miezi minne iliyopita, na kusema kweli sikufurahia. Kutokana na matatizo ya kifedha, tulikuwa tumepanga kumpata mtoto mmoja zaidi lakini baada ya mtoto wa pili kutimu miaka sita, hata hivyo mke wangu alishika mimba. Nahisi kana kwamba hajali hasa ikizingatiwa kwamba ni mimi peke yangu ninayefanya kazi. Kutokana na sababu kuwa hamakiniki na masuala ya kupanga uzazi, naweza kutumia mbinu zipi kama mwanamume, mbali na kutumia kondomu?

Ed, Nairobi

Mpendwa Ed,

Kwa mwanamume, mbinu za kupanga uzazi ni kuondoa uume ukeni kabla ya kumwaga manii, kuhasi (vasectomy) na kondomu. Katika mbinu ya kwanza, wakati wa kushiriki tendo la ndoa unapaswa kuondoa uume ukeni kabla ya kumwaga manii ili kuzuia yasiingie mle. Hata hivyo viwango vya kufeli ni takriban 22%. Katika mbinu ya kuhasi, daktari wa upasuaji hukata na kuziba mrija unaosafirisha manii. Baada ya miezi mitatu hakutakuwa na manii yatakayopita wakati wa ngono. Utaratibu huu huwa sahili na huchukua muda mfupi, hauna maumivu na kamwe hauathiri nguvu zako za kiume. Hata hivyo, ni vigumu kurejelea hali yako ya kawaida kwani inachukuliwa kuwa mbinu ya kudumu ya kupanga uzazi. Aidha, unaweza jizuia kushiriki ngono na mkeo wakati ambapo hayuko salama. Unaweza kufunzwa kufanya hivi katika kliniki ya afya ya uzazi. Mbinu zingine za kupanga uzazi bado zinafanyiwa utafiti ikiwa ni pamoja na tembe, sindano za wanaume miongoni mwa zingine.

 

Mpendwa Daktari,

Tangu utotoni nimekuwa nikikumbwa na masuala ya uzani. Mimi ni mwembamba sana ilhali marafiki zangu ni wanene. Mbinu zipi salama ambazo naweza kutumia kuongeza unene hasa katika sehemu ya makalio na kifua?

Lynn, Nairobi

Mpendwa Lynn,

Kuwa mwembamba zaidi kwa matamshi ya kimatibabu kunamaanisha kwamba kimo chako kikilinganishwa na uzani wako (BMI) kiko chini. Kiwango cha BMI cha kawaida ni kati ya 18.5 na 25. Ikiwa kiwango chako cha BMI kiko chini ya 18.5 basi unasemekana kuwa na uzani wa chini. Huenda hii ikasababishwa na jeni, au kwa sababu mwili wako unatumia nguvu nyingi kufanya kazi za kila siku. Aidha hali hii yaweza kutokana na sababu kwamba hauli chakula cha kutosha, au unajihusisha na shughuli nyingi. Pia yaweza kuwa ni kutokana na maradhi fulani au unakumbwa na tatizo la kiakili.

Huku baadhi ya watu wakiongeza au kupunguza uzani kuambatana na lishe au masuala mengine wanayokumbana nayo, uzani wa wengine haubadiliki kwa urahisi. Hii mara nyingi ni kutokana na jeni, hali ambayo kwa bahati mbaya haiwezi kubadilishwa. Ni vyema kuwa na uzani usiobadilika kila mara. Unapozidi kukomaa kiumri, itakuwa rahisi kuongeza uzani huku mfumo wako wa umetaboli ukipungua kasi. Dhana kwamba unene ni ishara ya afya njema ni potovu. Ikiwa uzani wako ni thabiti hasa katika kiwango kizuri kiafya, basi haupaswi kuingiwa na wasiwasi. Dumisha lishe bora, kula viwango vidogo vya vyakula kila mara, fanya mazoezi na jiepushe na tabia zisizoambatana na afya njema kama vile kuvuta sigara au kulewa kupindukia. Unaweza kutafuta ushauri kutoka kwa mtaalamu wa lishe atakayekushauri kuhusu vyakula vya kula na kwa viwango vipi. Hakuna jinsi ya kupima kwamba uzani unaoongeza utaelekea kwa kifua na makalio. Umbo la mwili wako hutegemea na jeni. Mafuta mengi mwilini yaweza kudhibitiwa kwa kuhakikisha lishe bora, vile vile mazoezi kupitia ushauri wa mkufunzi.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Afua kwa wanaougua kansa ya mapafu

SHANGAZI AKUJIBU: Alikuwa na nia gani kuniambia tukapimwe?

adminleo