Habari Mseto

Wakurugenzi wa KTDA wajitetea

October 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VITALIS KIMUTAI na CHARLES WASONGA

WAKURUGENZI 50 wa Shirika la Ustawishaji wa Kilimo cha Majinachai Nchini (KTDA) wamejitenga na changamoto zinazoikabili sekta hiyo na badala yake kulaumu siasa na kuzorota kwa bei ya zao hilo katika masoko.

Viongozi hao vilevile walisema wakulima walipata malipo duni kwa zao hilo mwaka 2019 kutokana na kushindwa kwa serikali kupata masoko mbadala ya majanichai kimataifa.

“Wakulima wa majanichai katika kaunti ya Bomet walipata mapato ya jumla ya Sh6.153 bilioni kutokana na kilo 42.675 milioni za majanichai katika mwaka wa kifedha uliopita. Kati ya pesa hizo, Sh3.04 bilioni zimekwisha kulipwa huku Sh1.96 bilioni zinazosalia ikitarajiwa zitalipwa mwishoni mwa mwezi huu,” akasema Bw Erick Langat, mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Majanichai cha Kapkoros baada ya kuongoza mkutano wa bodi hiyo Jumamosi katika mkahawa wa Brevan mjini Bomet.

Wanachama wa bodi hiyo pia walitaka wakulima wadogowadogo kukoma kung’oa mimea yao ya majanichai kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo hasa katika masoko ya kimataifa.

Katika wiki chache zilizopita, wakulima wengi wenye mashamba madogo madogo katika eneo hilo katika eneo hilo wamekuwa waking’oa mimea ya majani ili kutoa nafasi kwa upanzi wa mimea mingine wakidai KTDA na mawakala wengine wamekuwa wakiwapunja.

“Kama viongozi waliochaguliwa katika kaunti ya Bomet kuongoza sekta ya majani chai tunajikaza kusuluhisha changamoto zinazoikumba sekta hii. Tunaomba serikali na wanasiasa watuunge mkono ili tuweze kufaulu,” akasema Bw Langat.

Alisema ingawa kiwango cha uzalishaji majanichai nchini ni kilo 5.8 bilioni kwa mwaka, hitaji la zao hilo duniani ni kilo 5.6 biloni kwa mwaka na kupelekea kuwepo kwa kilo 200 milioni zaidi.

Wakurugenzi hao wa KTDA waliwataka viongozi waliochaguliwa kukoma kuingiza siasa katika changamoto zinazoikabili sekta hiyo na badala yake wabuni mbinu za kukabiliana na masaibu hayo, hasa namna ya kupata masoko mapya.

“Tunapinga miito kwa wakulima wang’oe mimea yao ya majanichai yao na kuwekeza katika shughuli zingine za kilimo kwani tuna matumaini kuwa hali itakuwa nzuri. Hii ni kwa sababu changamoto hizi zinaletwa na mabadiliko katika bei za chai katika masoko ya kimataifa kutokana na misukosuko ya kisiasa huko,” akasema Bw Langat.