Habari

Oparanya ashutumu wanaopinga juhudi za kufufua Mumias Sugar

October 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

GAVANA wa Kakamega Wycliffe Oparanya amewashutumu baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Magharibi kwa kupanga njama ya kusambaratisha juhudi za kufufua kiwanda cha sukari cha Mumias.

Bw Oparanya alidai Jumamosi kwamba kuna baadhi ya viongozi wanaotumiwa na baadhi ya watu mashuhuri kuhakikisha kiwanda hicho hakirejelei shughuli zake za kusaga miwa kama miaka ya nyuma.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Magavana, alitoa matamshi hayo katika uwanja wa Malinya eneobunge la Ikolomani, wakati wa ibada ya mazishi ya marehemu Adelaide Shikanga, mkewe aliyekuwa Seneta ya Kakamega Boni Khalwale.

“Wakiwa kwenye mikutano ya umma, wanasiasa hao hujifanya wanapigania ufufuaji wa kiwanda hiki lakini baadaye wao huweka mikakati na maadui kuhakikisha Mumias inasalia jinsi ilivyo kwa sasa,” akasema Bw Oparanya.

Matamshi ya Gavana huyo yalionekana kuwalenga wanasiasa ambao wamekuwa wakishinikiza rasilimali za kiwanda hicho ziuzwe kwa kiwanda kingine cha wamiliki binafsi.

Kaunti kusaidia

Hata hivyo, Bw Oparanya alishikilia kwamba serikali ya kaunti itaendeleza juhudi za kuhakikisha kiwanda hicho ambacho ni kitega uchumi kwa wakazi wa Magharibi, kinaendeleza shughuli zake.

“Tatizo hasa linasababishwa na viongozi wenzangu. Wamekataa kusema ukweli kuhusu jambo hilo na kazi yao kuu ni kuhadaa umma kuhusu yanayoendelea. Mumias imejipata katika hali yake ya sasa kutokana na domokaya ya wanasiasa kwenye hafla za mazishi,” akaongeza Bw Oparanya.

Aidha alishikilia kwamba Sh3.7 bilioni ambazo zilitolewa na serikali kusaidia katika kufufua kiwanda hicho hazitoshi kutokana na hasara kubwa iliyochangiwa na usimamizi mbaya wa miaka ya nyuma.

Aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa, naye alidai kwamba kuna mbunge ambaye amepokezwa kandarasi katika kiwanda hicho baada ya kuwekwa chini ya mrasimu wa benki ya KCB.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula alimwomba Bw Oparanya ambaye pia ni mwenyekiti wa jopokazi lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Novemba 2018 kuangazia changamoto ambazo zinaathiri viwanda vya sukari na namna ya kuvifufua.

Hivi majuzi, baadhi ya wakulima pia walilalamikia jinsi wanasiasa walivyoingilia suala hilo na kusema wana nia za kujinufaisha wao binafsi.