Operesheni kuitafuta bunduki ya afisa aliyeuawa Lamu yaendelea
Na KALUME KAZUNGU
OPERESHENI ya kusaka bunduki na risasi 60 zilizomilikiwa na afisa aliyeuawa kinyama eneo la Lamu Mashariki imeingia wiki yake ya tatu bila ya kuzaa matunda yoyote kufikia sasa.
Oktoba 2, 2019, afisa wa polisi wa cheo cha Konstebo, Hesbon Okemwa Anunda, aliripotiuwa kutoweka akiwa amebeba bunduki na risasi hizo 60 kabla ya mwili wake kupatikana siku tatu baadaye ukiwa umetupwa kwa kichaka karibu na barabara ya Kizingitini-Mbwajumwali.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, amesema Jumatatu kwamba huenda bunduki hiyo ikatumika vibaya endapo haitapatikana.
Bw Macharia amesema idara ya usalama, Kaunti ya Lamu ina imani kubwa kwamba bunduki hiyo haijavukishwa mpaka na kuingizwa nchi jirani ya Somalia bali iko mikononi mwa wananchi wa Lamu Mashariki.
Amewasihi wakazi kushirikiana na maafisa wa usalama na kutoa ripoti zitakazosaidia kupatikana kwa bunduki hiyo kabla haijatumika vibaya, ikiwemo kuendeleza wizi wa mabavu miongoni mwa jamii.
“Tumekuwa tukitafuta bunduki hiyo katika kipindi chote cha majuma mawili yaliyopita bila mafanikio. Bado hatujakufa moyo. Tunaendelea na operesheni kwenye vichaka, hasa sehemu ambapo mwili wa afisa wa polisi ulipatikana. Bunduki haijavukishwa nchini Somalia. Tuna imani kubwa kwamba bado iko mikononi mwa jamii. Tunawasihi kuitoa silaha hiyo kwani huenda ikatumika vibaya, ikiwemo kuendeleza wizi wa mabavu kwenye maeneo husika,” amesema Bw Macharia.
Mshukiwa
Kamishna huyo pia amesema hakuna mshukiwa yeyote ambaye kufikia sasa amekamatwa kuhusiana na mauaji ya afisa huyo wa polisi lakini akasisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea ili kubaini wahusika wa mauaji hayo.
“Hatujakamata yeyote kufikia sasa lakini tunajaribu kufuatilia mazungumzo ya simu; hasa kipindi cha mwishomwisho kabla ya afisa kuuawa. Tukiwapata waliozungumza naye tutawatia mbaroni na kuwauliza maswali kuhusiana na mauaji hayo,” akasema Bw Macharia.
Naye Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu Muchangi Kioi pia amethibitisha kwamba bunduki hiyo haijapatikana lakini akasisitiza kuwa operesheni bado inaendelea kote Lamu Mashariki.
“Bunduki bado haijapatikana lakini operesheni inaendelea bado. Tunasihi jamii kujitokeza na kutupa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa silaha hiyo,” akasema Bw Kioi.