Kimataifa

Matokeo ya awali vituoni yamuweka mbele mhafidhina Kais Saied

October 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

TUNIS, TUNISIA

RAIS mteule wa Tunisia kwa mujibu wa matokeo ya kura za awali, mtaalamu na mhafidhina Kais Saied, amewashukuru vijana nchini humo kwa kumpigia kura kwa wingi na kuchangia ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu ulioandaliwa Jumapili.

Rais Saied aliahidi kwamba atatekeleza mageuzi makubwa nchini humo baada ya kushinda zaidi ya asilimia 77 ya kura zote zilizokuwa zimehesabiwa.

“Tutajenga upya Tunisia. Vijana ndio waliongoza kampeni zangu na kuchangia ushindi huu,” akasema akihutubia halaiki ya wafuasi wake waliofurika kwenye makao makuu ya chama chake.

Imebainika kwamba Saied alipigiwa kura na vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 25 na wakagawana nusu bin nusu kura za wenye umri wa miaka 49 na zaidi na mpinzani wake, mwanahabari wa Nabil Karoui.

Aidha amesisitiza kwamba atatimiza ndoto ya wazalendo waliomng’oa madarakani Zine El Abidine Ben Ali ambaye alifariki juzi nchini Saudi Arabia alikokimbilia uhamishoni na akazikwa katika mji mtakatifu wa Mecca.