• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Wachungaji wa madhehebu tofauti waombea Thika Superhighway mjini Ruiru

Wachungaji wa madhehebu tofauti waombea Thika Superhighway mjini Ruiru

Na LAWRENCE ONGARO

MADEREVA wa magari kwenye barabara kuu ya Thika Superhighway wamehimizwa kuwa makini wanapoendesha vyombo hivyo vya usafiri katika nchi kavu.

Zaidi ya wachungaji 10 wa madhehebu tofauti kutoka Ruiru, Kaunti ya Kiambu mnamo wikendi walijumuika na wakazi wa Ruiru, katika eneo la Kwa Kairu mjini Ruiru ili kuitakasa barabara hiyo na kuiombea rasmi.

Maombi hayo yaliyoendelea kwa zaidi ya saa mbili yalijumusha wakazi wengi wa Ruiru na vitongoji vyake huku wakipongeza juhudi hiyo ya wachungaji.

Mmoja wa wachungaji hao – Charles Wachir – alisema malalamishi mengi ya wakazi wa Ruiru katika maeneo ya Kimbo, na Toll, yamekuwa ni watu kulalamika ya kwamba watu wengi wanaangamia kwa kugongwa kiholela na magari yanayopita sehemu hiyo kwa kasi inayopitiliza.

“Tumelazimika kufika hapa kama wachungaji kutakasa barabara hii ya Thika Superhighway ili watu wengi wasizidi kuangamia. Imekuwa ni msiba kwa wengi ambapo wamepoteza wapendwa wao hapa,” alisema mchungaji Wachira.

Kulemaa

Alitoa mfano ya wahudumu wengi wa bodaboda ambao wamepoteza maisha yao na wengine kuwa viwete.

Bw Ezekiel Teka, mkazi wa kijiji cha Murera, alisema ya kwamba wanaboda Boda wengi wameadhirika kutokana na ajali nyingi zinazopatikana katika eneo hilo.

“Kama hivi majuzi kuna mwanabodaboda alipata ajali mbaya alipogongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa Kasi. Kwa hivyo, siku ya leo tunafurahia kuona wachungaji wakiombea barabara hii ambayo imekuwa hatari kwa usalama,” alisema Bw Teka.

Alisema kwa chini ya kipindi cha miezi 10 sasa wanabodaboda wapatao watatu wamepoteza maisha yao kwa kugongwa na magari.

Aliiomba serikali ifanye hima kuona ya kwamba daraja la kisasa linajengwa eneo hilo ili kupunguza ajali zaidi kutokea.

Bi Wawiri Wamugo alisema wakazi wengi wamepitia masaibu mengi tangu kukamilika kwa barabara hiyo.

“Sehemu mbaya zaidi ni eneo la Kwa Kairu, ukielekea Kimbo, hadi eneo la Weighbridge karibu na kituo cha Toll mjini Ruiru. Maombi hayo ya leo ni muhimu sana kwa wakazi wa Ruiru na vitongoji vyake. Tungetaka maombi kama hayo yawe yakiletwa hapa kila mara,” alisema Bi Wamugo.

Alisema hata bewa la Ruiru Campus la Chuo Kikuu cha Kenyatta, wanafunzi wengi wa chuo hicho wamekuwa waathirika wa ajali mbaya wakijaribu kuvuka barabara hiyo.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) mwaka huu wa 2019 watu wapatao 2,591 wamepoteza maisha yao.

Kwa muda mrefu kumekuwa na pendekezo kuwe na daraja kubwa la kivukio katika eneo la Ruiru hasa Kwa Kairu kwa ajili ya wanafunzi wa chuo hicho na wakazi wake.

You can share this post!

Ruweida Obbo ashajiisha wanawake Lamu kuwa mstari wa mbele...

Githu ataka cheo cha Waziri Mkuu, naibu kibuniwe

adminleo