Wapwani walalama kuchezewa na serikali
Na MOHAMED AHMED
SERIKALI inaonekana kucheza mchezo wa paka na panya na washikadau wa shughuli za Bandari ya Mombasa kuhusiana na suala la usafirishaji wa mizigo.
Licha ya Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) kueleza kuwa wafanyabiashara wameruhusiwa kuchukua mizigo ili kuleta usawa wa kibiashara kati ya usafiri wa malori na reli ya kisasa (SGR), yanayoendelea Mombasa ni tofauti.
Hii ni kulingana na wafanyabiashara ambao wameilaumu serikali kuwa inawachezea shere na kutojali maslahi ya uchumi wa Pwani unaotegemea zaidi shughuli za Bandari.
Imebainika kuwa tofauti na tangazo kuwa wafanyabiashara wamepewa uhuru wa kuamua njia wanayotaka kutumia kusafirisha mizigo yao, wanaoleta mizigo nchini bado wanalazimika kutumia SGR.
Waziri wa Uchukuzi James Macharia wiki mbili zilizopita alisimamisha agizo la kusafirisha mizigo kwa SGR pekee akisema kuwa wafanyabiashara wako huru kuchagua usafirishaji wa mizigo yao kwa SGR ama malori.
Mwenyekiti wa Fast Action Business Community, Salim Karama alisema kuwa tangu Bw Macharia kusimamisha agizo kuhusu SGR, ni kontena chache sana ambazo zimesafirishwa kwa malori.
“Kuna baadhi ya CFS ambazo zinapata kontena sita pekee. Ni vipi kontena hizo zitatosheleza kupeana kazi kwa wakazi wa hapa? Uhuru wa kibiashara bado haujaruhusiwa na hatutaki wakazi wetu wachezewe,” akasema Bw Karama.
Mwenyekiti wa Muungano wa Uhifadhi wa Makasha (KIFWA), Roy Mwanthi pia alisisitiza kuwa hakukuwa na mizigo yoyote ambayo inapelekwa Nairobi kwa malori.
Wadokezi wa Taifa Leo walieleza kuwa kontena chache ambazo ziliruhusiwa kusafirishwa kwa malori baada ya tangazo la Bw Macharia ni zile ambazo zilikuwa zinasafirishwa katika Kaunti ya Mombasa pekee.
Lakini Jumanne, mkuu wa mawasiliano wa KPA, Bernard Osero alisisitiza kuwa malori yapo na uhuru wa kuchukua mizigo katika bandari ya Mombasa.