Moto nyumbani kwa Raila
Na RICHARD MUNGUTI
MVUTANO umezuka katika familia ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuhusiana na urithi wa mali ya mwanawe aliyeaga dunia, Fidel Castrol Odinga.
Kutokana na mvutano huo, mkewe Bi Ida Odinga na kitinda mimba wake Winnie Odinga wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakiomba kushirikishwa katika usimamizi wa mali iliyokuwa ikimilikiwa na Fidel.
Wawili hao pia wanaomba kufutiliwa mbali kwa kibali ambacho mjane wake Fidel, Lwam Getachew Bekele alipewa na mahakama mnamo Januari 9 mwaka huu cha kusimamia mali ya mwendazake.
Kati ya hoja ambazo ziliwasilishwa mahakamani Jumatano mbele ya Jaji Aggrey Muchelule, Bi Ida na Winnie wanasema mjane huyo aliwaacha nje ya urithi wavulana wawili pacha ambao wanadai Fidel alizaa na mwanamke mwingine nje ya ndoa.
Jaji Muchelule aliagiza uchunguzi wa DNA ufanyiwe pacha hao ili kuthibitisha iwapo Fidel ndiye alikuwa baba yao.
Kulingana na hati ya kiapo ya Bi Ida na Winnie, pacha hao walizaliwa Juni 1, 2015, miezi mitano baada ya Fidel kuaga dunia Februari 4, 2015.
Waliongeza kuwa Fidel alikuwa ‘akiwatunza’ pacha hao alipokuwa hai, suala ambalo Bi Lwam kwenye majibu yake anashangaa ilikuwaje ilhalli hawakuwa wamezaliwa akiwa hai.
Bi Lwam pia anagusia kuhusu kujikanganya kwa Bi Ida na Winnie kwa kudai Fidel alikuwa baba wa watoto hao pacha na hali kwenye sehemu nyingine ya hati yao ya kiapo wanasema mwanawe Bi Lwam ndiye uzao pekee alioacha marehemu.
Bi Lwam anaendelea kusema kuwa hati za kuzaliwa za pacha hao hazionyeshi jina la baba yao.
“Lakini kama itathibitishwa kuwa pacha hao walizaliwa na marehemu, nitawajumuisha katika urithi wa mali ya marehemu,” anasema Bi Lwam.
Fidel alifariki kabla ya kuandika wosia kuhusu urithi wa mali yake, hali ambayo sasa imezua mvutano katika familia ya waziri mkuu wa zamani.
Kati ya mali ambayo imeorodheshwa kuwa ilimilikiwa na Fidel ni nyumba katika eneo la Tipuana Park mtaani Karen, vipande viwili vya ardhi Kisumu na kingine Kajiado, hisa katika kampuni ya Axum na Ambesa, magari manne na akaunti za benki.
Bi Ida na kitinda mimba wake wanadai kuwa mjane wa Fidel hakuorodhesha magari matatu ya kifahari, akaunti tatu za benki na nyumba yao kwenye nakala za korti.
Wanaendelea kudai kuwa familia ya Bw Odinga ilijaribu kuwasiliana na Bi Lwam na nduguye Fahm Getachew Bekele ili waweze kuomba usimamizi wa pamoja wa mali ya Fidel, lakini hawakufanikiwa.
Ombi kupewa usimamizi wa mali
Wanasema Bi Lwam aliwasilisha kisiri ombi mahakamani la kupewa usimamizi wa mali ya mwendazake na hivyo kuwaacha nje wahusika wengine wa Fidel, na kuwa hawezi kuaminika kusimamia mali hiyo kwa njia ifaayo.
Pia wanaeleza hofu kuwa mjane huyo ambaye ana uraia wa Kenya, Eritrea na Amerika anaweza kutoroka nchini.
Bi Ida na Winnie wanadai kuwa tayari Bi Lwam ameanza kuharibu mali ya Fidel na kwa hivyo wanaomba kushirikishwa katika usimamizi ili kulinda mali hiyo kwa ajili ya watoto walioachwa na marehemu, na kuhakikisha mali hiyo imegawa ifaavyo.
Pia wanadai kuwa mara baada ya mazishi ya Fidel, Bi Lwam alitoroka nyumbani walimokuwa wakiishi na Fidel katika mtaa wa Karen na pia akasitisha mawasiliano na familia ya Bw Odinga.
Wanaendelea kulalamika kuwa Bi Lwam alimwondoa mwanawe waliyezaa na Fidel kutoka shule na kumzuia asitangamane na familia ya Bw Odinga, madai ambayo mjane huyo amekanusha.
Akijibu, Bi Lwam anasema kutokana na kuwa ndiye mjane wa marehemu, sheria inampa kipaumbele cha kusimamia mali ya mumewe.
Pia anasema walalamishi walichelewa kuwasilisha pingamizi zao kortini katika muda unaokubalika kisheria.
“Madai ya walaolamishi ni ya uwongo na yenye nia mbaya. Mlalamishi wa kwanza (Ida) ndiye aliye na ripoti ya upasuaji wa maiti. Amekuwa akitoa madai ya uwongo dhidi ya familia yangu, marafiki na mimi binafsi,” Bi Lwam anasema.