• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sonko amtaka Rais asimamie Nairobi

Sonko amtaka Rais asimamie Nairobi

Na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Nairobi, Bw Mike Sonko sasa anamtaka Rais Uhuru Kenyatta achukue sehemu ya usimamizi wa kaunti hiyo iliyo jiji kuu la taifa.

Bw Sonko alimlalamikia Rais kwamba matapeli wamemlemea katika serikali ya kaunti kwa kiasi cha kutisha.

Alikuwa akizungumza Jumatano wakati Rais Kenyatta alizindua ujenzi wa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA, hadi eneo la Westlands, Nairobi.

“Makundi ya wawekezaji matapeli katika kaunti ni makubwa zaidi na ninahitaji msaada wako kuyavunja,” gavana huyo akamwambia Rais.

Alisema yuko radhi kuruhusu serikali kuu ichukue usimamizi wa idara mbalimbali muhimu za kaunti ikiwemo ya kukusanya ushuru na ile ya mipango ya kaunti, kama hilo ndilo litawezesha ufisadi kukomeshwa Nairobi.

Hata hivyo, wito wake huenda usiwezekane kutekelezwa kwani katiba inaeleza wazi kuhusu ugavi wa majukumu kati ya serikali kuu na za kaunti.

“Hatua hii ikichukuliwa, makundi hayo yatavunjwa na mwananchi atapata huduma bora ipasavyo,” akasema.

Changamoto kuu ambazo Bw Sonko alisema zinakumba utawala wake kutokana na ufisadi wa baadhi ya maafisa wake ni kama vile unyakuzi wa ardhi za walalahoi na utoaji vibali vya ujenzi wa majumba yasiyofikia kiwango kinachofaa cha usalama.

Alitoa mfano wa ardhi iliyo eneo la Mukuru ambayo serikali ilikuwa imeagiza mwaka wa 2015 igawanywe kwa maskwota, lakini baadaye kukatokea mwekezaji wa kibinafsi aliyeenda kortini kusema ardhi ilikuwa yake.

Bw Sonko alidai bwanyenye huyo, ambaye hakutajwa, alikuwa amewasilisha stakabadhi feki na hivyo basi inafaa Rais aingilie kati kwani agizo la kukabidhi vipande vya ardhi kwa maskwota lilitoka kwake.

Rais Kenyatta alimwagiza kamishna wa eneo la Nairobi achunguze madai hayo ya Bw Sonko na kuwasilisha ripoti kwake leo Alhamisi.

Kufuata wanasiasa kikondoo

Rais alitoa wito kwa wananchi hasa vijana wasikubali kufuata wanasiasa kikondoo na kuchochewa kuanzisha vita dhidi ya wenzao kwa misingi ya kisiasa.

“Tulishindana na Raila lakini hiyo haimaanishi yeye ni adui yangu. Kushindana ni sawa lakini kuishi ni pamoja,” akasema.

Alisisitiza kuhusu hitaji la jamii kuheshimu wanawake kwa kusema: “Nyinyi vijana kama mnataka mwanamke, hamstahili kwenda kumkosea heshima. Wewe nenda utongoze polepole. Ukibahatika sawa, ukikosa tafuta mwingine.”

Rais Kenyatta ambaye baadaye alizindua awamu ya pili ya SGR itakayotoka Nairobi hadi Naivasha alipuuzilia mbali wanaotilia shaka miradi yake ya maendeleo na kusema ana maono kuhusu mahali anakotaka Kenya iwe miaka 50 ijayo.

Aliongoza pia shughuli ya kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Makasha ya Shehena mjini Naivasha.

Kwa sasa ujenzi wa awamu ya pili ya SGR imepitia vituo vya Ongata Rongai, Ngong, Mai Mahiu na Suswa, ikihofiwa ufadhili haujapatikana kuendeleza ujenzi huo hadi Naivasha inavyokusudiwa.

You can share this post!

Uchaguzi wa wakurugenzi KTDA wakumbwa na utata

Pasta mpenda pesa abaki bila waumini

adminleo