Habari

Sakaja aelezea kutoridhishwa kwake na kuteuliwa kwa Mary Wambui

October 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nairobi Johnson Sakaja ni kiongozi wa hivi punde kuonekana kupinga uteuzi wa aliyekuwa mbunge wa Othaya Mary Wambui kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Ajira (NEA).

Bw Sakaja amekuwa jijini Belgrade nchini Serbia kuwakilisha Kenya katika Kongamano la Umoja wa Mabunge (Inter Parliamentary Union) anasema hakufurahishwa na uteuzi huo.

“Ni fahari yangu kuwakilisha Kenya katika kongamano ya muungano wa mabubunge unaoendelea hapa Belgrade, Serbia. Niwawakilisha vizuri hata kama huo uteuzi haukutufurahisha,” Sakaja akasema kupitia chapisho katika ukurasa wa akaunti yake ya Twitter huku akirejelea uteuzi wa Bi Wambui.

Seneta Sakaja ndiye alidhamini mswada ambao ulipelekea kubuniwa kwa mamlaka ya NEA. Sheria hiyo ilipitishwa bungeni na kutiwa saini na Rais Uhuru Kenya mnamo 2016. Wakati huo Bw Sakaja alikuwa akihudumu katika mbunge maalum katika bunge la kitaifa na mwenyekiti wa muungano wa wabunge vijana (KYPA).

Alipobuni mswada huo, Seneta Sakaja mwenye umri wa miaka 34, alidhamiria kuwa Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Ajira (NEA) ingeweka misingi maalumu kuhusu uzalishaji wa ajira, haswa kwa vijana.

Mamlaka hiyo pia ingeshirikisha masuala yote kuhusu ajira nchini kwa ushirikiano na sekta ya umma na ile sekta binafsi.

Lakini saa chacha baada ya waziri wa Leba Ukur Yatani kuchapisha notisi katika gazeti rasmi la serikali kutangaza uteuzi wa Bi Wambui mwenye umri wa miaka 69, Wakenya walikosoa hatua hiyo wakisema mtu mwenye umri wa chini angepewa nafasi hiyo.

Alielekezewa lawama ni Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake kwa ujumla.

Sasa Alhamisi, amedokeza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kwamba amewaambia mawakili wake pamoja na wale wa Muungano wa Wanasiasa Chipukizi Bungeni kuwasilisha kesi mahakamani kuwashtaki Waziri wa Leba, Mwanasheria Mkuu na aliyekuwa mbunge wa Othaya Mary Wambui Munene.

Miongoni mwa waliopinga uteuzi huo ni Seneta Maalum Millicent Omanga, wakili Donald Kipkorir na mwanaharakati wa upinzani anayeishi uhamishoni nchini Canada aliko pia na uraia Miguna Miguna.

Miguna alifurushwa kutoka nchini Kenya.

Hata hivyo, Bi Wambui alitetea uteuzi wake akisema ana uwezo wa kutekeleza kazi hiyo.

“Nilipata uteuzi huu kwa sababu ninafaa kuliko wanaolalamika. Nina tajiriba ya kutosha kutekeleza majukumu ya afisi hiyo kwa manufaa ya Wakenya wote, hasa vijana wetu,” akasema.

Na Jumatano Rais Kenyatta alitetea hatua ya kuteuliwa kwa Bi Wambui huku akitoa wito kwa vijana kuwaheshimu wanawake na viongozi waliotwikwa wajibu wa kusimamia asasi mbalimbali.

Alikuwa akihutubu katika eneo la Suswa alipozindua awamu ya 2A ya Reli ya Kisasa (SGR) ya hudumu ya uchukuzi wa treni kutoka Ngong’ hadi Suswa.