Habari Mseto

Maafisa walioshiriki sensa walalamikia kukosa malipo

October 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WANGARI

KUNDI la maafisa wapatao 50 walioshiriki shughuli ya kuhesabu watu Agosti liliandamana Alhamisi kulalamikia dhidi ya kukosa kulipwa ujira wao baada ya kufanya kazi.

Maafisa hao wakiongozwa na Bw Gerald Nandwa walisema kuwa walikuwa wamechoka kuzungushwa na maafisa wa Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS), ambao wamekuwa wakiwakwepa kila wanapoulizia pesa zao.

“Hatujalipwa tangu shughuli ya kuhesabu watu ilipoisha. Wamekuwa wakituzungusha huku na kule. Wengine wao wamezima simu huku wengine wakitueleza wao si wafanyakazi wa KNBS. Hatujui sasa tumwendee nani,” alisema Bw Nandwa.

Kulingana na Bw Nandwa, waandamanaji hao walihusisha maafisa kutoka kaunti mbalimbali nchini walioshiriki kazi hiyo na ambao bado hawajapokea malipo yao hadi sasa.

“Watu wa Nairobi walilipwa kitambo lakini kuna baadhi ambao bado hawajapokea hela zao. Maeneo ya Kakamega unapata kwa mfano Kakamega Kusini wamelipwa lakini maeneo mengine bado hawajapata mishahara yao hadi tunashangaa wanafanya mambo haya vipi,” akalalama.

Hata hivyo, tuliwasiliana na Mkurugenzi wa KNBS Bw Zachary Mwangi aliyekanusha madai hayo akisema ni kaunti tano pekee ambazo hazikuwa zimelipwa ambapo watakuwa wametuma pesa kufikia Jumanne wiki ijayo.

“Tunaendelea kulipa watu, tumebakisha kaunti tano ambazo kufikia Jumatatu au Jumanne watakuwa wamepokea pesa zao. Wanaosema hawajapokea pesa Kaunti ya Nairobi ni wale walioandika akaunti ambazo hazifanyi kazi ambapo tukituma pesa zinakosa kwenda. Pia kuna wale ambao hawakurejesha vifaa tulivyowapa,” alisema Bw Mwangi akiongeza kuwa maafisa wake walikuwa wakishughulikia suala hilo.

Kwa upande wake, Bw Nandwa alieleza kuwa suala la kupoteza au kutorejesha vifaa halikuwa hoja maadamu tayari walikuwa wameafikiana jinsi ya kusuluhisha jambo hilo.

“Ikiwa kuna kifaa kilichopotezwa walikuwa wakate kiasi fulani cha pesa. Kama ni tarakilishi walikuwa wakate Sh15000 kutoka kwa mshahara au kama ni kuvunja kioo chake ungekatwa Sh5000. Lakini kuna waliorejesha kila kitu na bado hawajapokea malipo yao,” alilalama.