Wiper yalambishwa sakafu huku ODM, Jubilee ziking’aa
Na KITAVI MUTUA, CHARLES LWANGA na CHARLES WASONGA
UMAARUFU wa Chama cha Wiper eneo la Ukambani ulitikiswa kiliposhindwa kwenye uchaguzi mdogo wa wadi ya Mutonguni, kaunti ya Kitui na chama cha Maendeleo Chap Chap huku vyama vya ODM na Jubilee vikishinda chaguzi ndogo za udiwani Malindi na Marsabit.
Uchaguzi wa wadi ya Mutonguni uliochukuliwa kama wa kupimana nguvu kati ya viongozi wa vyama hivyo, Kalonzo Musyoka na Alfred Mutua ambao wamekuwa wakipigania ubabe wa kisiasa eneo hilo.
Mhandisi Musee Mati wa Maendeleo Chap Chap (MCC) alizoa kura 2,892 huku mgombeaji wa Wiper Stephen Kithuka akifuata kwa karibu kwa kupata kura 2,147.
Kushindwa kwa Wiper kumesawiriwa kuwa pigo kwa Musyoka ambaye ni kigogo wa siasa katika eneo zima la Ukambani na anatoka kaunti ya Kitui.
Bw Musyoka mwenyewe alifahamu hilo kabla ya uchaguzi huo na ndio maana aliongoza kampeni za kumpigia debe Bw Kithuka akiwasihi wapiga kura wasimwaibishe nyumbani kwa kumkataa mgombeaji wa Wiper.
Chama cha ODM kilishinda uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda kaunti ya Kilifi.
Ushindi wa Reuben Katana umefasiriwa kama pigo kwa mustakabali wa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ambaye ametangaza kuwa atawania ugavana wa Kilifi kwenye uchaguzi Mkuu wa 2022.
Bw Katana alitangazwa mshindi kwa kuzoa kura 4,177 na kumshinda Abdulrahman Mohamed Omar aliyepata kura 2,331.
Bi Jumwa alikuwa akimuunga mkono Bw Mohammed ambaye aliwania kiti hicho kama mgombeaji huru baada ya kugura ODM.
Nacho chama cha Jubilee kilishinda kiti cha udiwani wa wadi ya Loiyangalani, kaunti ya Marsabit katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi.
Mgombeaji cha chama hicho tawala Stephen Nakeno alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1,522 akifuatwa kwa karibu na Lesiantam Iltele wa Kanu aliyepata kura 1,048.
Mgombeaji wa chama cha Maendeleo Chap Chap Titus Lolmogut Lenguro alikuwa wa tatu kwa kupata kura 663 akifuatia na Tobias Chodow Lenguro wa ODM aliyepata kura 306.