• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Mshukiwa wa ugaidi akanusha madai mahakamani

Mshukiwa wa ugaidi akanusha madai mahakamani

Na BRIAN OCHARO, MISHI GONGO na JOSEPH NDUNDA

MSHUKIWA wa ugaidi anayedaiwa kuwa na mizizi yake Syria, Somalia na nchi zingine tatu, amekanusha madai ya kuhusika na njama pamoja na utekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na Pwani.

Salim Aboud Khalid alikanusha mashtaka hayo Jumanne katika mahakama ya Mombasa.

Maafisa wa kupambana na ugaidi walieleza korti kuwa Bw Khalid ambaye ameepuka mitego kadha, amekuwa katika orodha ya watu wanaosakwa sana na polisi kuanzia Juni 2018 kufuatia madai ya kuhusika na kundi la al-Shabaab.

“Mshukiwa amekuwa akikwepa maafisa wa polisi. Tumekuwa tukimchunguza kwa madai ya kupanga mashambulio katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na Pwani,” alisema afisa wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi Bw Dickson Indaru.

Mshukiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kuwa katika kundi la al-Shabaab na kuzuia maafisa wa polisi kutekeleza kazi zao. Pia alidaiwa kujaribu kumshambulia Konsteboli wa polisi, Edapal Lowasa kwa kisu.

Hakimu Mkuu, Bi Edna Nyaloti alielezwa kuwa mshukiwa akiwa na nia ya kutekeleza mauaji, alijaribu kumdunga kisu afisa huyo wa polisi mnamo Septemba 11. Kulingana na maafisa hao waliiomba mahakama kumnyima mshukiwa dhamana wakidai kuwa mshukiwa huenda akakosa kufika mahakamani akiachiliwa kwa dhamana.

Walisema mshukiwa alitorokea Tanzania ambako alikuwa akijificha tangu 2013 baada ya wenzake wawili kupigwa risasi na kuuawa jijini Mombasa.

Pia waliambia korti kuwa awali kulikuwa na njama ya kutekeleza mashambulio ya kigaidi katika kanda ya Pwani ambayo yanadaiwa kupangwa na kundi la kigaidi , mshukiwa akiwa miongoni mwao.

“Kuna uwezekano wa mshukiwa kutoroka vikao vya mahakama ikizingatiwa kuwa alikuwa mafichoni tangu mwaka wa 2013,” walieleza korti.

Mahakama ilielezwa kuwa Bw Khalid pia alikuwa anachunguzwa kuhusu madai ya kuhusika kwake katika visa vya uhalifu, ambavyo ni pamoja na wizi wa pesa. Kesi hiyo itatajwa Oktoba 30.

Kwingineko, mwanamume mwenye umri wa miaka 22, ambaye alitisha kumuua mkewe waliyetengana, Jumanne alishtakiwa kwa kosa la kuharibu mali baada ya kuingia nyumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu.

Bw Elmelick Okari, ambaye hufanya kazi za vibarua, alishtakiwa katika mahakama ya Makadara, Nairobi kwa kuvunja vioo vya dirisha vyenye thamani ya Sh5,000 baada ya kuvamia nyumba ya Bi Mercy Kemunto Ondieki katika mtaa wa Mathare, mnamo Oktoba 28 mwaka huu.

Aidha, anakabiliwa na shtaka la kutisha kumuua Bi Ondieki.

Anadaiwa kusema hivi: “Sharti nimuue Mercy na baada ya hapo niko tayari kupelekwa jela. Sitaki kumwona maishani mwangu.” Alitoa matamshi hayo kabla ya kuvunja mlango wake na kuingia kwa nguvu alipodinda kufungua.

Jumanne, alikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu, Marisa Opondo huku akidai kuwa walikuwa wameoana kwa miaka miwili na wakajaaliwa mtoto mmoja aliyefariki.

“Tunaweza kuridhiana na kuishi pamoja kwa sababu bado namchukulia kuwa mke wangu,” akasema Bw Okari.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000 pesa taslimu. Kesi hiyo itasikizwa Machi 9, 2020.

You can share this post!

Waziri Matiang’i afungua KCPE kwa maombi

Jaji azuia bajeti ya mahakama kupunguzwa

adminleo