• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Sera mpya ya Twitter kupiga marufuku matangazo ya kisiasa

Sera mpya ya Twitter kupiga marufuku matangazo ya kisiasa

Na MARY WANGARI na MASHIRIKA

WANASIASA wanaotumia mitandao ya kijamii kuvutia wapigakura wamepata pigo kuu kufuatia hatua ya usimamizi wa mtandao maarufu wa kijamii wa Twitter kutangaza utatoa rasmi sera ya kupiga marufuku matangazo ya kisiasa Novemba 15, 2019, na utekelezwaji wake uanze Novemba 22.

Kupitia ukurasa wa akaunti yake ya Twitter, mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Twitter, Jack Dorsey alitangaza Jumatano hatua hiyo muhimu inayotazamiwa kuwaathiri sio tu wanasiasa nchini bali kote duniani, ambao wamekuwa wakitumia mtandao huo mashuhuri kutangaza ajenda zao kisiasa, kusimanga wapinzani wao na muhimu kuwashawishi wapigakura.

“Tumefanya uamuzi wa kukomesha matangazo yote ya kisiasa kupitia Twitter kote ulimwenguni. Tunaamini ujumbe wa kisiasa unapaswa kupitishwa kwa njia ya haki na wala sio kununuliwa,” alisema Dorsey.

Kulingana na bosi huyo wa Twitter hatua hiyo ilidhamiriwa kuzuia wanasiasa dhidi ya kutumia vibaya mtandao huo kuwashawishi wapiga kura kufanya maamuzi yasiyofaa, ambayo hatimaye yataathiri maisha ya mamilioni ya watu.

“Japo matangazo ya mitandao yana nguvu mno na yenye matokeo makuu kwa watangazaji wanaotoza malipo, uwezo huo husababisha hatari kuu kisiasa ambapo unaweza kutumika kutoa ushawishi katika upigaji kura hali itakayoathiri maisha ya mamilioni,”

“Hii haihusu uhuru wa kujieleza. Inahusu kulipa ili kufikia hadhira. Na kulipa ili kuongeza uwezo wa kuwasilisha ujumbe kisiasa una matokeo muhimu ambayo miundomsingi ya sasa kidemokrasia huweza isiwe tayari kukabiliana nayo,” alihoji.

Huku akifafanua kuhusu hatua hiyo ambayo haitaathiri jumbe kuhusu usajili wa wapiga kura, Dorsey alisisitiza kwamba matangazo ya kisiasa “huzua changamoto mpya kabisa kwa mijadala ya umma: usawazishaji wa jumbe kutokana na mafunzo kimtambo na ulengaji kidijitali, habari za kupotosha zisizodhibitiwa, na uongo mwingi. Yote katika kasi na kiwango cha juu mno na upana usio wa kawaida,”

Huku akimtania mkurugenzi wa Facebook Mark Zuckerberg ambaye tasnia yake tajika imekashifiwa kwa kuruhusu wanasiasa kuwahadaa wapigakura kupitia matangazo; ya uongo yakiwemo, Dorsey alisema kampuni yake hata hivyo, italegeza kamba endapo mwanasiasa atakuwa anastahili zaidi kunufaika kupitia jukwaa hilo.

“Tunajitahidi kuwazuia watu dhidi ya kutumia vibaya mitambo yetu kueneza habari za uongo, lakini ikiwa mtu atatulipa kulenga na kuwalazimisha watu kuona matangazo yao ya siasa, wanaweza kusema chochote watakacho!”

You can share this post!

‘Dimbwi la Clayworks lingali tishio kwa wakazi’

Afisa wa GSU anayedaiwa kuua atupwa rumande siku 21

adminleo