Tutamshinda Raila asubuhi na mapema Kibra – Ruto
Na SAMUEL BAYA na KITAVI MUTUA
NAIBU Rais Dkt William Ruto amesema Jumamosi kwamba chama cha Jubilee kitashinda kwa kishindo chama cha ODM kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge unaotarajiwa kufanyika Alhamisi ijayo eneobunge la Kibra.
Akiongea katika soko la Salgaa, Kaunti ya Nakuru baada ya kuchangia makanisa 22, Dkt Ruto amesema kuwa ni kutokana na hofu ya kushindwa ODM imeanza kulalamika mapema kwa Tume Huru ya Uchaguzi nchini na kutoa makataa, matakwa na masharti mbalimbali.
“Huko kambini kwa ‘baba’ hali sio shwari na ndio maana mmeona katika siku za hivi karibuni wanalia na kulalamika bila mpango. Hiyo ni dalili ya mtu aliyeshindwa mapema. Kwa uwezo wa Mungu na akitupa uhai na hasa tukiangalia maendeleo ambayo tumefanya Kibra kama Jubilee, mbunge wa Jubilee atachaguliwa mapema asubuhi,” alisema Dkt Ruto.
Akaongeza: “Tutashinda Kibra tena kwa kura nyingi sana.”
Alikuwa ameandamana na Seneta wa Nakuru Susan Kihika, Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Nakuru, Bi Liz Chelule, mbunge wa Molo Bw Kimani Kuria, mbunge wa Bahati Bw Kimani Ngunjiri, mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki Bw David Gikaria na madiwani kadha.
“Ukweli ni kuwa Bw Odinga hakuweza kuendeleza Kibra kimaendeleo katika miaka yote ambayo alikuwa mbunge. Ile miradi yote ambayo hakuweza kuiendeleza kwa muda huo sasa imetekelezwa na serikali ya Jubilee,” alisema naibu huyo wa Rais.
ODM yapigwa jeki
Wakati huo huo, ODM imepigwa jeki magavana watatu wa Ukambani walipomuunga mgombeaji wake Imran Okoth.
Jumamosi, Gavana wa Machakos Alfred Mutua na Charity Ngilu wa Kitui wamekutana na Bw Odinga na kutangaza kuwa watampigia debe Imran.
Jamii ya Wakamba ndiyo ya tatu kwa wingi katika eneobunge la Kibra, baada ya Waluo na Waluhya, hali inayowaweka katika nafasi ya kuamua mshindi katika kinyang’anyiro cha Alhamisi.
Kwa kusaka usaidizi kutoka kwa Dkt Mutua ambaye ni kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC) na Bi Ngilu, Bw Odinga analenga kuyeyusha ushawishi wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka anayeunga mgombea wa chama cha Ford Kenya Khamisi Butichi.
Dkt Mutua amethibitisha kwamba yeye na Bw Odinga wamekuwa wakijadiliana wanavyoweza kushirikiana sio tu katika uchaguzi mdogo wa Kibra lakini katika mpango mpana wa kupalilia maridhiano nchini kupitia jopokazi la BBI.