• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Seneta akemea wanaomhepa Ruto

Seneta akemea wanaomhepa Ruto

SAMUEL BAYA na MERCY KOSKEY

SENETA wa Nakuru, Bi Susan Kihika , amekashifu viongozi wa kaunti waliokosa kuhudhuria hafla iliyosimamiwa na Naibu Rais William Ruto wikendi.

Alipoandamana na Dkt Ruto katika soko la Salgaa, Kaunti ya Nakuru kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuchangisha fedha kwa makanisa ya eneo hilo Jumamosi, alisema ni jambo la kusikitisha kwamba hakuna hata afisa mmoja wa serikali ya kaunti ambaye alifika katika kikao hicho.

Kulingana naye, maafisa wa kaunti wangechangia kutoa mwongozo wa jinsi ambavyo serikali kuu na ya kaunti zinaweza kushirikiana kuboresha miundo msingi katika eneo hilo.

“Inavunja moyo kuona kwamba katika hafla hii ambayo naibu wa Rais amefika Salgaa hakuna mwakilishi hata mmoja wa serikali ya kaunti. Kama Gavana au naibu wake angelikuwa hapa, tungeweza kuongea naye kuona jinsi gani serikali ya kitaifa itashirikiana na ile ya kaunti kuangalia jinsi ambavyo mpango wa kutengeneza mabomba ya maji taka na egesho la magari la Salgaa ingelifanyika,” akasema Seneta huyo.

Katika kile ambacho kilionekana kama mpango wake wa kuubeza utawala wa Gavana Lee Kinyanjui, Bi Kihika aliitaka kaunti kuhakikisha kwamba miradi ambayo inafaa kufaidi wananchi inaendelezwa bila matatizo yoyote.

“Kuna shida kubwa katika miundo msingi ya mji huu wa Salgaa. Hakuna mabomba ya maji taka hapa Salgaa, pamoja na kukosekana kwa egesho la magari katika kituo hiki cha biashara,” akasema Bi Kihika.

Vile vile, Seneta huyo aliitaka serikali ya kaunti kutoa hatimiliki ya ardhi ya ekari tano katika eneo la Visoi ili hospitali iweze kujengwa.

“Katika eneo hili hakuna hata zanahati na tumejua ile shida ambayo tuko nayo ya ajali katika eneo hili. Tunaomba mpango huo usaidie,” akasema Bi Kihika.

Alimuomba naibu wa Rais asaidie kuanzisha ujenzi wa shule katika eneo la Salgaa ambapo alidai hakuna shule hata moja, licha ya kuwa na wakazi wengi ambao idadi yao inaendelea kuongezeka.

Mwakilishi wa kike katika kaunti hiyo, Bi Liz Chelule pia aliitaka serikali kuhakikisha kwamba ujenzi wa hospitali ya Salgaa unaanza kwa sababu ni muhimu sana.

“Kuna ekari sita za hospitali ya Salgaa ambazo zimekuwa tu bila ujenzi kuanza. Tunaomba hili suala liwe litaangaliwa vyema kwa sababu afya ni muhimu sana katika eneo hili,” akasema Bi Chelule.

You can share this post!

Kalonzo azidi kutengwa na viongozi Ukambani

Ndege waharibifu walivyoangamizwa Mwea

adminleo